Maandamano ya "Vizibao vya Njano" yafanyika kwa wiki ya 18 Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i52211-maandamano_ya_vizibao_vya_njano_yafanyika_kwa_wiki_ya_18_ufaransa
Maandamano ya vugu vugu la "Vizibao vya Njano" yameendelea katika mitaa ya mji mkuu wa Ufaransa, Paris na miji mingine ya nchi hiyo kwa wiki ya 18 mfululizo huku waandamanaji wakiyataja maandamano ya jana kuwa ya "Makataa."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 17, 2019 01:13 UTC
  • Maandamano ya

Maandamano ya vugu vugu la "Vizibao vya Njano" yameendelea katika mitaa ya mji mkuu wa Ufaransa, Paris na miji mingine ya nchi hiyo kwa wiki ya 18 mfululizo huku waandamanaji wakiyataja maandamano ya jana kuwa ya "Makataa."

Kwa mujibu wa taarifa, waandamanaji walijitokeza kwa wingi katika barabara muhimu za Paris, ikiwemo barabara muhimu ya Avenue des Champs-Élysées ambapo polisi walikabiliana na waandamanaji hao.

Aidha maandamano sawa na hayo yameripotiwa katika miji mingine kadhaa ya nchi hiyo  kama vile Strasbourg, Lille, Marseille, Bordeaux, Toulouse na Lyon ambapo washiriki wameendelea kubainisha upinzani wao dhidi ya serikali ya nchi hiyo.

Harakati ya "Vizibao vya Njano" ilianza kufanya maandamano tarehe 17 mwezi Novemba mwaka jana kupinga mipango ya kiuchumi inayotekelezwa na serikali ya Ufaransa ikiwemo hatua ya kupandisha kodi ya nishati. Hadi sasa polisi ya Ufaransa imethibitisha kuuawa watu kumi kwenye maandamano hayo. 

Rais Macron wa Ufaransa ameshindwa kuzima vugu vugu la "Vizibao vya Njano"

Wananchi wa Ufaransa wanashiriki katika maandamano hayo ya kila Jumamosi kote nchini humo  kupinga mfumo wa ubepari na sera za kiuchumi za Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo.

Wafanya maandamano hao wanamtambua Macron kuwa Rais tajiri na wanaamini kwamba siasa za kiuchumi za rais huyo na kutotilia maanani matakwa ya wananchi wake ndiyo chanzo cha kushuhudiwa matatizo ya kiuchumi na kuenea dhulma na uonevu nchini Ufaransa.