Ankara: Marekani ichague ama kushirikiana na Uturuki au magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i52619-ankara_marekani_ichague_ama_kushirikiana_na_uturuki_au_magaidi
Makamu wa Rais wa Uturuki amejibu matamshi ya Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence, ambaye aliitaka Ankara inunue ndege za kivita za F-35 kutoka Marekani badala ya kununua mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya makombora wa S-400 kutoka kwa Russia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 04, 2019 03:23 UTC
  • Ankara: Marekani ichague ama kushirikiana na Uturuki au magaidi

Makamu wa Rais wa Uturuki amejibu matamshi ya Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence, ambaye aliitaka Ankara inunue ndege za kivita za F-35 kutoka Marekani badala ya kununua mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya makombora wa S-400 kutoka kwa Russia.

Akitoa radimali yake kwa kauli hiyo ya Pence, Fuat Oktay,  Makamu wa Rais wa Uturuki ameiambia Marekani kwamba, wakati umefika ichague ima kushirikiana na Uturuki ambayo ni mwanachama mwenzake katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO, au magenge ya kigaidi.

Makamu wa Rais wa Uturuki ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa, "Marekani lazima ichague. Je inataka kuendelea kuwa muitifaki wa Uturuki, au iko tayari kuuza urafiki wetu kwa kuungana na magenge ya kigaidi yanayohatarisha usalama na ulinzi wa mwanachama mwenzake wa NATO?"

Mapema jana, Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence alisema Uturuki sharti ichague iwapo inataka kusalia kuwa mshirika muhimu wa NATO au kujiweka katika hatari ya kupokonywa uanachama kwa 'maamuzi yake ya kipumbavu' kama kununua mfumo wa ngao ya makombora wa S-400 kutoka Russia.

Uturuki inasisitiza kuwa iko huru kununua silaha inazohitaji kutoka kwa waitifaki wake

Hivi karibuni msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, alitoa onyo kali kwa Uturuki akitishia kuwa Ankara itakumbwa na hali mbaya iwapo itanunua silaha hizo kutoka kwa Russia, na kwamba eti hatua hiyo itazusha mgogoro mkubwa katika uhusiano wa kiulinzi wa Ankara na Washington.

Mara kwa mara, Rais Recep Tayyib Erdogan wa Uturuki amekuwa akisisitizia msimamo wa nchi yake wa kununua mfumo huo wa kujilinda na mashambulizi ya makombora kutoka kwa Russia bila ya masharti akisisitiza kuwa, mfumo huo ni kwa manufaa ya usalama wa taifa la Uturuki.