Siasa za kimaonyesho za Trump za kuitaka Iran ifanye mazungumzo naye
Katika kipindi cha masaa 24 tokea Iran itangaze rasmi kwamba itapunguza ushirikiano wake na pande husika katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, rais wa Marekani ameitaka Iran mara tatu, ifanye mazungumzo naye.
Akizungumza jana Alkhamisi mbele ya waandishi habari, Rais Donald Trump amesema: 'Ninapenda viongozi wa Iran wanipigie simu. Wanapasa kupiga simu na iwapo watatekeleza hilo, sisi tuko tayari kufanya nao mazungumzo.'
Ni wazi kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na hasa baada ya Marekani kujitoa katika mazugumzo ya nyuklia ya Iran mashuhuri kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA, viongozi wa nchi hiyo wamedai mara nyingi kwamba wako tayari kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuitaka irejee kwenye maeza ya mazungumzo. Hii ni katika hali ambayo Marekani hivi karibuni ilijitoa kwenye meza ya mazungumzo ya nyuklia na kukataa kutekeleza ahadi zake kuhusiana na mazungumzo hayo. Hivyo nchi inayopasa kurejea kwenye meza ya mazungumzo ni Marekani na wala sio Iran.
Jambo la pili ni kwamba kabla ya kufanyika mazungumzo yoyote ya pande mbili, kuna mazingira ya lazima yanayopasa kuandaliwa kabla ya kufanyika mazungumzo hayo, likiwemo suala la kujiepusha kufanyiana dharau, udhalilishaji na vitisho. Katika miezi ya hivi karibuni watawala wa Marekani mbali na kutoa matamshi ya dharau na tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran wameongeza vitisho vya kijeshi dhidi ya nchi hii kwa kadiri kwamba wametuma katika Ghuba ya Uajemi manowari iliyobeba ndege za kivita aina ya B-52 na kusema kuwa hilo ni onyo kwa Iran.
Katika upande wa pili, kwa kujitoa katika mapatano ya JCPOA Marekani imeithibitishia kivitendo Iran na nchi nyingine za dunia kwamba nchi hiyo si ya kuaminika kuhusiana na ahadi inazotoa. Hivi sasa kuna wasiwasi mkubwa kwamba mapatano yoyote yanayofikiwa kati ya Marekani na upande wa pili yanaweza kubatilishwa wakati wowote na rais wa hivi sasa wa nchi hiyo au marais wengine watakaoingia madarakani baada yake. Ni ukweli huo ndio uliopelekea kuvunjika kwa duru mbili za mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Trump na viongozi wa Korea Kaskazini. Hivyo kabla ya kufanyika mazungumzo yoyote kati ya Iran au nchi nyingine yoyote na Marekani, kwanza hatua muhimu zinapaswa kuchukuliwa kwa shabaha ya kujenga imani upande wa watawala wa Marekani na kuhakikisha kuwa hawatakariri tena tabia na mienendo ya kushangaza ya rais kigeugeu wa hivi sasa wa nchi hiyo.
Kwa vyovyote vile, matukio ya miaka kadhaa iliyopita ya Marekani yanathibitisha wazi kwamba marais wa nchi hiyo, uwe ni utawala wa Wademocrat kama ilivyokuwa katika kipindi cha Barack Obama au wa Warepublican kama ilivyo sasa katika utawala wa Donald Trump, hawana uwezo wa kutosha wa kutekeleza ahadi wanazotoa kwa pande wanazofanya nazo mazungumzo. Kuhusu ukweli huo, Seneta Tom Cotton anasema kama tunavyomnukuu kuhusiana na mswada uliowasilishwa na baadhi ya maseneta wa Marekani kuhusiana na uwezekano wa kuondelewa vikwazo dhidi ya Iran: 'Vikwazo haviwezi kuondolewa na rais kupitia 'kalamu na simu tu'.'
Kwa maneno mengine ni kuwa, iwpo mswada huo utapitishwa rais wa hivi sasa na marais wengine wote watakaokuja wa Marekani hatakuwa na uwezo wa kutekeleza ahadi wanazotoa katika mazungumzo bali ni wajumbe 535 wa kongresi ya nchi hiyo ndio watakaokuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo. Kwa kutilia maanani ushindani na mvutano mkubwa wa kisiasa uliopo kati ya vyama viwili vya Democrats na Republicans katika kongresi hiyo itakuwa vigumu kufikiwa mapatano kati ya vyama hivyo na rais anayetawala kuhusiana na suala lolote muhimu la kitaifa au kimataifa.
Kwa vyovyote vile, ni wazi kuwa bila ya kubadilishwa maneno ya dharau na vitisho ya watawala wa Marekani, kujengwa imani, na muhimu zaidi, kuwa na uwezo wa kutosha wa kutekeleza ahadi zinazotolewa na watawala hao, litakuwa ni jambo lisilo la kimantiki kuendelea kusisitiza na kudhani kwamba inatosha kwa Iran kumpigia simu Trump na hapo matatizo yote ya hivi sasa yaliyosababishwa na Marekani yatakuwa yametatuliwa.