Amnesty: Ufaransa haiaminiki tena kwa kuendelea kuiuzia silaha Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53393-amnesty_ufaransa_haiaminiki_tena_kwa_kuendelea_kuiuzia_silaha_saudia
Shirika la kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Ufaransa isitishe uuzaji wa silaha zake kwa Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen, likisisitiza kuwa serikali ya Paris haiaminiki tena kwa madai yake kwamba silaha hizo hazitumiki dhidi ya raia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2019 09:09 UTC
  • Amnesty: Ufaransa haiaminiki tena kwa kuendelea kuiuzia silaha Saudia

Shirika la kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Ufaransa isitishe uuzaji wa silaha zake kwa Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen, likisisitiza kuwa serikali ya Paris haiaminiki tena kwa madai yake kwamba silaha hizo hazitumiki dhidi ya raia.

Aymeric Elluin, afisa wa Amnesty International anayesimamia masuala ya silaha na sheria za kimataifa amesema, "Ufaransa inatoa matamshi ya kukinzana. Mwanzo walisema hakuna silaha zao Yemen, kisha wakasema silaha zao nchini Yemen zinatumika kwa ajili ya kujihami tu, lakini dunia sasa inafahamu kuwa silaha hizo zinatumika kinyume na sheria ya haki za binadamu."

Amesisitiza kuwa jamii ya kimataifa haiwezi kuamini kauli ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ambaye hivi karibuni alisema silaha za nchi yake nchini Yemen hazitumiki dhidi ya raia.

Hapo jana watetezi wa haki za binadamu walijaribu kuzuia bila mafanikio upakiaji wa shehena za silaha za Ufaransa kwenye meli ya Saudia kaskazini mwa Ufaransa. 

Hujuma za Saudia Yemen kwa kutumia silaha za Wamagharibi

Saudi Arabia ikiungwa mkono na kusaidiwa na Marekani, Imarati, Israel na washirika wao wengine na kwa kutumia silaha za nchi za Magharibi hususan Uingereza, ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi.

Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo na mashambulizi hayo yamesababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua maelfu ya raia wasio na hatia. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha katika vita hivyo.