Uingereza, Ujerumani: Ulaya inafanya juhudi za kutekeleza mfumo wa INSTEX
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53411-uingereza_ujerumani_ulaya_inafanya_juhudi_za_kutekeleza_mfumo_wa_instex
Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimesema zinafanya juu chini kuhakikisha kuwa mfumo maalumu wa kifedha wa Ulaya na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (INSTEX) unaanza kufanya kazi.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
May 11, 2019 03:26 UTC
  • Uingereza, Ujerumani: Ulaya inafanya juhudi za kutekeleza mfumo wa INSTEX

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimesema zinafanya juu chini kuhakikisha kuwa mfumo maalumu wa kifedha wa Ulaya na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (INSTEX) unaanza kufanya kazi.

Richard Moore, Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya kisiasa katika Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza amesema, "Serikali ya London itaendelea kufungamana na makubaliano ya nyuklia, na itajitahidi kuhakikisha kuwa  mfumo maalumu wa kifedha wa Ulaya na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (INSTEX) unatekelezwa."

Naye Maria Adebahr, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani alisema jana Ijumaa kuwa, nchi kubwa za Ulaya zinafanya kila linalowezekana ili kufanikisha utekelezwaji wa mfumo huo wa mababilishano ya fedha.

Kabla ya hapo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema nchi zilizosaini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA zina wajibu wa kufungamana na mapatano hayo ya kimataifa.

Mfumo wa INSTEX

Tarehe 31 Januari mwaka huu Umoja wa Ulaya na baada ya miezi kadhaa ya majadiliano na Tehran, hatimaye ulianzisha mfumo huo maalumu wa kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliopewa jina la  (INSTEX) ingawa tangu wakati huo EU imekuwa ikichelewesha utekelezwaji wa mfumo huo kwa visingizio mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo, Rais Hassan Rouhani wa Iran siku ya Jumatano alisema kwamba Tehran imesitisha utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya JCPOA, kukiwemo kuongeza akiba ya urani yake iliyorutubishwa pamoja na maji mazito ya nyuklia na kama katika kipindi cha siku 60 nchi za Ulaya zitashindwa kuchukua hatua za kukabiliana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, basi Tehran itachukua hatua zaidi.