India na Pakistan zatangaza azma ya kutatua tofauti baina yao
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa India na Pakistan wametangaza azma ya kutatua tofauti za nchi zao kufuatia mgogoro ulioibuka hivi karibuni.
Shah Mehmood Qureshi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan na Sushma Swaraj, Waziri wa Mambo ya Nje wa India wameyasema hayo baada ya kukutana kando ya mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje la Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai huko Bishkek, mji mkuu wa Kyrgyzstan (SCO.) Katika mkutano huo Shah Mehmood Qureshi amesema kuwa, Islamabad daima imejiandaa kuanza mazungumzo na serikali ya New Delhi. Aidha amesisitizia azma ya serikali ya Pakistan ya kutatua tofauti za ndani na nchi jirani yake ya India kupitia njia ya mazungumzo.
Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wa ngazi ya juu wa India na Pakistan kukutana katika mazungumzo yasiyo rasmi yapata miezi mitatu iliyopita tangu kulipoibuka mapigano kati ya nchi mbili. Duru mpya ya mzozo katika uhusiano wa India na Pakistan iliibuka baada shambulio la kigaidi lililotokea katika eneo la Kashmir lililo chini ya udhibiti wa India, ambalo lilipelekea kwa akali askari 44 wa India kuuawa. Serikali ya New Delhi inaamini kwamba hujuma hiyo ilitekelezwa na kundi la kigaidi la Jaishu-Muhammad lililoko ndani ya ardhi ya Pakistan. Baada ya hujuma hiyo ya kigaidi, ndege za kivita za India zilifanya mashambulizi makubwa ya ulipizaji kisasi katika maeneo ya Pakistan na hivyo kuziingiza nchi hizo katika mvutano zaidi.