Seneta: Trump anatumia Iran kama kisingizio cha kuiuzia Saudia mabomu zaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53676-seneta_trump_anatumia_iran_kama_kisingizio_cha_kuiuzia_saudia_mabomu_zaidi
Seneta mmoja wa Marekani ameonya kuwa, yumkini Rais Donald Trump akatumia kisingizio cha taharuki kati ya nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama kisingizo cha kuiuzia Saudi Arabia mabomu mapya, bila idhini ya Kongresi ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 23, 2019 23:13 UTC
  • Seneta: Trump anatumia Iran kama kisingizio cha kuiuzia Saudia mabomu zaidi

Seneta mmoja wa Marekani ameonya kuwa, yumkini Rais Donald Trump akatumia kisingizio cha taharuki kati ya nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama kisingizo cha kuiuzia Saudi Arabia mabomu mapya, bila idhini ya Kongresi ya nchi hiyo.

Chris Murphy, Seneta wa Connecticut wa chama cha Democrat amesema kuna uwezekano mkubwa utawala wa Trump utumie taharuki ambayo imeipalilia yenyewe kati yake na Iran kuhalalisha mauzo mapya ya silaha za Marekani kwa utawala wa Riyadh.

Seneta huyo ambaye pia ni mwanachama wa Kamati ya Uhusiano wa Kigeni ya Seneti ya Marekani amesema, "Nimeskia kwamba Trump anapanga kutumia kasoro zilizopo kwenye Sheria ya Kudhibiti Silaha ili kuidhinisha mauzo makubwa ya mabomu kwa Saudia, kwa njia ambayo Kongresi haitakuwa na sauti ya kusimamisha mauzo hayo."

Kwa mujibu wa sheria hiyo, Kongresi ya Marekani sharti ipewe siku 30 ili iidhinishe mauzo ya silaha kwa nchi ajinabi, na pia ina uwezo wa kubatilisha mauzo hayo ikiwa itahisi inakiuka sheria yenyewe.

Saudia, ng'ombe wa kukamuliwa na Marekani

Ifahamike kuwa, Saudia ndiye mteja mkubwa zaidi wa silaha za Marekani duniani, ambapo kufikia sasa tokeo mwaka 2009, imenunua silaha zenye thamani ya dola bilioni 129 kutoka Washington.

Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita, shirika la Amnesty International na mashirika mengine mawili ya haki za binadamu yalilalamikia vikali kuendelea kuuziwa silaha Saudi Arabia na wavamizi wengine wa Yemen, yakisisitiza kuwa Riyadh inatumia silaha hizo kufanya jinai za kivita.