Narendra Modi apata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu India
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53685-narendra_modi_apata_ushindi_mkubwa_katika_uchaguzi_mkuu_india
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu uliochukua zaidi ya mwezi mmoja ambapo watu takribani milioni 600 walipiga kura.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 24, 2019 03:44 UTC
  • Narendra Modi apata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu India

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu uliochukua zaidi ya mwezi mmoja ambapo watu takribani milioni 600 walipiga kura.

Kwa mujibu wa taarifa, chama cha Bharatiya Janata cha Modi kimeshinda zaidi ya viti  300 kati ya viti 543 vya bunge la nchi hiyo.

Modi mwenye umri wa miaka 68, ametembelea makao makuu ya chama chake kusherehekea ushindi huu katika taifa hilo lenye demokrasia kubwa duniani.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Waziri Mkuu Mondi amewashukuru raia wa nchi hiyo kwa kumrejesha madarakani kuongoza kwa muhula mwingine wa miaka mitano, na kuahidi kuwa ushindi huo umempa nguvu ya kufanya bidii zaidi. Tayari chama kikuu cha upinzani cha Congress, ambacho kimejishindia viti 49 pekee, kinachoongozwa na Rahul Gandhi kimekubali kushindwa.

Rahul Gandhi amekubali kushindwa katika uchaguzi mkuu India

Kushindwa huko kunahesabiwa kuwa fedheha kubwa ikizingatiwa kwa vizazi vingi, chama hicho kimekuwa na ushawishi mkubwa nchini humo na kiliongozwa na wazee wake Rahul Gandhi waliowahi kuwa mawaziri wakuu.

Waziri Mkuu wa nchi jirani ya Pakistan Imran Khan amempongeza Modi kwa ushindi huo, na ameahidi kushirikiana naye kuhusu amani na maendeleo ya kanda ya kusini mwa Asia.