Ushindi wa Modi katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa India
Chama tawala cha Bharatiya Janata Party BJP cha nchini India kinachoongozwa na Narendra Modi kimepata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa hivi karibuni wa bunge kwa kujizolea viti 343 kati ya viti vyote 542 vya bunge hilo.
Chama hicho kimepata ushindi huo dhidi ya vyama pinzani kutokana na sera zake za kutekeleza ahadi kilizotoa kuhusiana na mauala ya kuimarisha uchumi wa nchi, kutoa vipaumbele kwa raia wa India na kuchukua misimamo mikali kuhusu masuala ya usalama wa taifa.
Katika uchaguzi wa mwaka 2014 chama cha BJP kilipata ushindi pia kwa kujinyakulia viti 282. Tokea mwaka 1984 hadi sasa hakuna chama chochote ambacho kilikuwa kimewahi kushinda uchaguzi mara mbili mfululizo na kupata wingi wa viti bungeni. Watu karibu milioni 900 walikuwa wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huo ambapo walitakiwa kuwachagua wabunge 542 wa bunge la India. Kila chama au muungano wa kisiasa nchini humo unatakiwa kupata kwa uchache wingi wa viti 272 ili uweze kuunda serikali.
Ushindi huu wa pili mfululizo wa chama tawala cha BJP katika uchaguzi wa bunge la India tokea uchaguzi wa 2014 ni jambo lililotarajiwa. Moja ya sababu za ushindi mkubwa wa chama hicho, ni kutokuwepo mshindani mwenye nguvu dhidi ya chama cha BJP na hasa baada ya kudhoofika chama kikuu cha upinzani cha Congress ya Taifa katika miaka mitano iliyopita.
Chama cha Congress ya Taifa ambacho ni mshindani mkuu wa chama tawala cha BJP katika kipindi cha tangu mwaka 2014 hadi mwaka huu wa 2019 hakikuweza kukosoa siasa na utekelezaji wa serikali ya Modi wala kuwabainishia Wahindi udhaifu wa serikali hiyo katika baadhi ya mambo, ili kudhoofisha nafasi ya chama hicho tawala mbele ya fikra za waliowengi nchini humo.
Kuna mtazamo huu kwamba chama cha Congress ya Taifa katika miaka mitano iliyopita kilishindwa kabisa kuwa na nafasi ya chama cha upinzani nchini India kwa ajili ya kukosoa na kurekebisha siasa na utendaji wa serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi na badala yake kuchukua misimamo ya kihamasa tu isiyozingatia mantiki wala ukweli wa mambo na hivyo kudhoofisha nafasi yake kama mbadala mzuri wa chama tawala cha BJP mbele ya waanchi wa India.
Chama cha BJP ambacho katika uchaguzi uliopitana baada ya kupita miongo mitatu kilifanikiwa kubuni serikali ya kwanza kikiwa peke yake kilikuwa kimepata nguvu maradufu ya kuweza kukipa ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa hivi karibuni, na hivyo kuongeza umashuhuri wake nchini humo kwa kujiongezea viti 61 zaidi ikilinganishwa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2014.
Pamoja na hayo Modi pia katika miaka mitano iliyopita amekuwa akikosolewa na wapinzani wake kutokana na serikali yake kushindwa kutekeleza ahadi za kiuchumi kupitia nara yake ya kampeni za uchaguzi ya 'Ujenzi wa India." Waziri Mkuu huyo alikuwa amewaahidi Wahindi nafasi zaidi za ajira na kuimarisha uchumi wa nchi hiyo, jambo ambalo halikufanikiwa sana. Katika miaka michache iliyopita, India imekabiliwa na tatizo la kupungua ukuaji wa uchumi wake na nafasi za ajira jambo ambalo liliwapa wapinzani fursa nzuri ya kukosoa na kushambulia serikali yake.
Licha ya mafanikio madogo aliyopata katika kutekeleza ahadi zake alizozitoa katika uchaguzi wa 2014 lakini ushindi mkubwa kilioupata chama cha BJP katika uchaguzi wa mara hii, unathibitisha wazi kwamba wananchi wa India wameamua kumpa fursa nyingine Waziri Mkuu Modi, ali apate nafasi mpya ya kuweza kuendelea kutekeleza nara yake ya 'Ujenzi wa India' aliyotoa mwaka 2014 katika mfumo mpya wa 'Maendelea Endelevu' ambayo ilikuwa nara yake ya uchaguzi wa mwaka huu. Wanataraji kwamba katika miaka mitano ijayo, suala hilo litamuwezesha kutekeleza sera za kuibadilisha nchi hiyo kuwa kituo muhimu cha kimataifa cha uzalishaji bidhaa na uvutiaji uwekezaji wa kigeni.