UN yakosoa vizingiti vya utawala wa Trump dhidi ya Zarif
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54794-un_yakosoa_vizingiti_vya_utawala_wa_trump_dhidi_ya_zarif
Umoja wa Mataifa umekosoa vikali hatua ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani ya kumwekea vizingiti Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javad Zarif.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 16, 2019 07:49 UTC
  • UN yakosoa vizingiti vya utawala wa Trump dhidi ya Zarif

Umoja wa Mataifa umekosoa vikali hatua ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani ya kumwekea vizingiti Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javad Zarif.

Farhan Haq, Naibu Msemaji wa UN amesema umoja huo unatiwa wasiwasi na vizingiti vya usafiri vilivyowekwa na utawala wa Trump dhidi ya Zarif ambaye yuko Marekani.

Dakta Zarif yuko Marekani kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha kila mwaka cha viongozi wa ngazi za juu wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameeleza bayana kuwa, "UN imeitaarifu Washington kuhusu wasiwasi wake wa nchi mwenyeji kumwekea vikwazo vya kusafiri mwanadiplomasia huyo."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javad Zarif

Wakati huohuo, Tehran imesema vizingiti hivyo vya kumzuia Zarif asisafiri baina ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa na Ofisi ya uwakilishi wa Iran katika UN au makazi ya balozi wa Iran katika umoja huo havitaathiri ratiba ya kazi ya Dakta Zarif. 

Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, "Kumzuia asitembee katika baadhi ya barabara za mjini New York bila shaka hakutavuruga ratiba yake ya kazi. 

Mwezi uliopita, utawala wa Trump ulitishia kumwekea vikwazo Dakta Zarif lakini ukasimamishe tena mpango huo bila kutoa ufafanuzi wa kina.