Trump avunja rekodi ya kusema uongo
Kanali ya televisheni ya CNN imeanzisha kampeni maalumu ya kutathmini ukweli na uongo wa matamshi anayotoa rais wa Marekani Donald Trump na kuripoti kuwa katika muda wa wiki moja iliyopita kiongozi huyo amesema uongo mara 61.
Tovuti ya kanali hiyo ya televisheni imeripoti kuwa, CNN imeanzisha kampeni ya kupima ukweli na uongo wa madai yanayotolewa na Trump na kutangaza kuwa wiki iliyopita rais huyo wa Marekani alitoa madai 61 yasiyo sahihi na ya uongo.
Ripoti ya CNN imeongeza kuwa, katika hotuba zake kwa umma, Trump huchanganya maelezo yake na mambo yasiyo sahihi, hukuza mambo na kutia chumvi na hata husema maneno makubwa ya uongo.
Kanali hiyo ya televisheni nchini Marekani imesema, inapasa wapiga kura wa nchi hiyo wafahamu jinsi rais wao anavyowadanganya na kuwahadaa na ikabainisha kwamba, kuanzia sasa na kuendelea, itakuwa kila wiki inatangaza na kuwapatia watazamaji wake takwimu za madai yasiyo sahihi na ya kauli za uongo anazotoa Trump hadharani; iwe ni katika hotuba au jumbe zake za Twitter.
Kanali ya televisheni ya CNN imeashiria pia ripoti ya uchunguzi iliowahi kufanya huko nyuma na kueleza kwamba, tangu Trump aingie Ikulu ya White House na kushika hatamu za urais wa Marekani Januari 2017 hadi mwezi Mei mwaka huu wa 2019, kwa wastani amekuwa akisema uongo takribani mara sita kwa siku.
Gazeti la Washington Post, nalo pia liliwahi kutoa ripoti baada ya Donald Trump kuanza kipindi chake cha urais, kuhusiana na madai yasiyo sahihi na hata ya uongo aliyokuwa akitoa mara kwa mara kuhusu masuala ya ndani na nje ya nchi, na likatangaza kwamba, katika kila muda wa masaa 24, Trump husema uongo mara nane.../