Idadi ya wabunge wa Marekani wanaotaka Trump auzuliwe inazidi kuongezeka
Idadi ya wajumbe wa chama cha Democrat katika Baraza la Wawakilishi la Marekani wanaotaka rais wa nchi hiyo Donald Trump asailiwe kwa lengo la kumuuzulu imeongezeka baada ya wajumbe wengine wanne kuunga mkono hoja hiyo.
David Cicilline, mjumbe wa jimbo la Rhode Island, Pramila Jayapal anayewakilisha jimbo la Washington, Mary Gay Scanlon wa jimbo la Pennsylvania na Veronica Escobar mwakilishi wa jimbo la Texas, ambao wote ni wajumbe wa kamati ya sheria ya Baraza la Wawakilishi la Marekani wameeleza katika tamko lao lililochapishwa na gazeti la Atlantic kwamba wanafuatilia mchakato wa kumsaili Trump kwa lengo la kumuuzulu.
Baada ya ushahidi wa Robert Mueller, aliyeongoza uchunguzi wa madai ya kuingilia Russia uchaguzi wa rais wa Marekani wa mwaka 2016, wawakilishi hao wanne wa chama cha Democrat wametangaza kuwa: kamati yao imewasilisha dai mahakamani la kuwawezesha kupata nyaraka za baraza la waamuzi kuhusu ripoti ya Mueller.
Katika maelezo aliyotoa siku ya Jumatano iliyopita mbele ya kamati ya sheria na kamati ya usalama za Baraza la Wawakilishi, Robert Mueller alisisitiza kwa mara nyingine kuwa, uchunguzi uliofanywa hauthibitishi kwamba timu ya kampeni za uchaguzi ya Trump ilikula njama pamoja na Russia.
Hata hivyo Mueller alibainisha pia kwamba, upo uwezekano wa Trump kupatikana na hatia ya makosa baada ya kumalizika kipindi chake cha urais.
Tangu ilipotolewa ripoti rasmi ya uchunguzi huo uliofanywa na Robert Mueller, mjadala wa kutaka rais wa Marekani asailiwe kwa lengo la kumuuzulu umezidi kupamba moto na kupata nguvu miongoni mwa wabunge wa nchi hiyo.../