Washington Post: Trump ni jinamizi baya zaidi kwa demokrasia
Gazeti la Washington Post limemtaja rais wa Marekani Donald Trump kuwa ni jinamizi baya zaidi linaloitambalia demokrasia ya nchi hiyo.
Gazeti hilo linalochapishwa nchini Marekani limeandika katika toleo lake la leo kuwa, Trump anajaribu kutumia maneno na misamiati itakayozusha mfarakano.
Washington Post limeongeza kuwa: Hasama na chuki za ubaguzi wa rangi zimekuwapo ndani ya Marekani tokea hapo kabla na zinatokota chini kwa chini katika jamii ya nchi hiyo, lakini tangu Trump alipoingia katika ulimwengu wa siasa amekuwa akizitumia tofauti hizo na ubaguzi wa rangi kama silaha ya kisiasa kufanikishia malengo yake.
Katika matamshi mapya ya kibaguzi na ya kuchochea mifarakano aliyotoa, rais huyo wa Marekani amemtukana Elijah Cummings, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la nchi hiyo mwenye asili ya Kiafrika na kuliita jimbo lake la Baltimore kuwa ni "soko lililochafuka na kufurika mapanya".
Katika jumbe za kibaguzi alizoandika katika siku za karibuni kwenye ukurasa wake wa Twitter, rais wa Marekani amewatukana matusi ya kibaguzi wabunge wanawake wa chama wa Democrat katika Kongresi ya nchi hiyo kwa kuwaambia, wao si Wamarekani na kuwataka warudi nchi walizotoka.
Wabunge wanawake aliowalenga Trump kwa matamshi hayo ya chuki za kibaguzi ni Ilhan Omar aliyezaliwa Somalia, RashidaTlaib mwenye asili ya Palestina, Alexandria Ocasio-Cortez ambaye asili yake ni Puerto Rico na Ayanna Pressley, Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika.../