Kujiuzulu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Taifa wa Marekani
Tangu Donald Trump aliposhika hatamu za kuongoza Marekkani alianza kutekeleza sera ya kuwafukuza kazi na hata kuwalazimisha maafisa wa ikulu ya White House wajiengue wenyewe.
Sambamba na hayo baadhi ya maafsia wa serikali ya Washington waliamua kujiuzulu kama njia ya kuonesha malalamiko yao dhidi ya siasa na sera za Trump na mfano wa yote hayo ni kufukuzwa kwa aliyekuwa waziri wa mambo ya nje Rex Tillerson na kulazimishwa kujiuzulu aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Marekani, James Mattis.
Mlolongo wa kujiuzulu au kulazimishwa kujiuzulu maafisa wa ngazi za juu wa Marekani bado unaendelea. Katika uwanja huo Dan Coats Mkurugenzi wa Upelelezi wa Taifa (DNI) wa Marekani atajiuzulu nafasi hiyo siku chache ziijazo. Coats amekuwa katika nafasi hiyo tangu mwezi Machi mwaka 2017. Alfajiri ya Jumatatu ya jana tarehe 29 Julai Donald Trump alithibitisha kwamba, Dan Coats atajiuzulu na kwamba nafasi yake itachukuliwa na John Ratcliffe. Trump alisema katika ujumbe wake wa Twitter kwamba: "John Ratcliffe ambaye ni mbunge wa chama cha Republican katika jimbo la Texas ameteuliwa kuwa Mkurugenzi mpya wa Upelekezi wa Taifa. Kipindi cha Dan Coats kama Mkurugenzi wa Upelelezi wa Taifa kitahitimishwa tarehe 15 Agosti na nina furaha kutangaza kwamba, Ratcliffe ndiye atakayeshika nafasi hiyo".
John Ratcliffe ni mjumbe wa sasa wa Kamati ya Idara ya Mahakama ya Congresi ya Marekani na miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Trump, na vilevile ni mpinzani mkubwa wa kazi na shughuli za Robert Mueller anayechunguza faili la uchaguzi wa rais wa mwaka 2016.
Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza habari hiyo ya kubadilishwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Taifa wakati gazeti la New York Times limeandika kuwa: Mkurugenzi wa Upelelezi wa Taifa atatangaza kujiuzulu kwake katika siku chache zijazo kwa sababu ya kutoridhika kwa taasisi za upelelezi za Marekani kuhusiana na utendaji wa serikali ya Trump.
Dan Coats ni mashuhuri sana kwa kuwa na misimamo mikali dhidi ya Russia. Hata hivyo anajulikana kuwa na misimamo tofauti na ya Donald Trump kuhusiana na Iran na Korea Kaskazini. Coats alisema Januari 2019 katika kikao cha Kongresi ya Marekani kwamba: Ni jambo lililombali Korea Kaskazini kutupilia mbali silaha zake za nyuklia. Vilevile anaamini kwamba, kuna udharura wa kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baina ya Iran na nchi za kundi la 5+1. Hii ni licha ya kwamba, Trump ni mpinzani mkubwa zaidi wa makubaliano hayo na anafanya kila awezalo kuhakikisha kwamba yanavunjwa na kusambaratishwa.
Kujiuzulu kwa Dan Coats kunaonesha kuwa, Donald Trump ambaye ni mashuhuri kwa kiburi, udikteta na kutokubali maoni ya watu wengine, hawezi kustahamimili mitazamo na maoni ya wapinzani wake, na kutokana na nafasi yake kama Rais wa Marekani anawaweka kando maafisa na viongozi wasiokubaliana na maoni yake. Kwa kadiri kwamba, hadi sasa maafisa zaidi ya 60 wa serikali wametimuliwa au kujiuzulu. Kwa utaratibu huo kipindi cha utawala wa Donald Trump nchini Marekani kitaendelea kukumbukwa na Wamarekani wengi kutokana na mwenendo huo usio na kifani.
Trump ni mwepesi sana wa kuwaajiri maafisa na kisha kuwatimua baada ya kipindi kifupi sana, na muda wa kuhudumu baadhi ya maafisa hao katika Ikulu ya White House huishia katika kipindi cha siku kadhaa tu! Mbali na idadi ya maafisa wanaotimuliwa, idadi ya maafisa wa swerikali wanaojiuzulu pia inazidi kuongezeka. Maafisa hao wanaojiuzulu kwa hakika hawaafikiani au kwa maneno sahihi zaidi, wanapinga fikra, siasa na mitazamo ya kiongozi huyo.
Wakati huo huo utendaji mbaya wa Donald Trump umewafanya wanasiasa na maafisa wa zamani na wa sasa wa Marekani na hata wabunge wa nchi hiyo watoa wito wa kukabiliana na kiongozi huyo kutokana na tabia yake ya kutumia vibaya madaraka na kuwafuta wapinzani wake. Jerrold Nadler ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Idara ya Mahakama za Marekani katika Kongresi ya nchi hiyo anasema: "Tunaweza kumtambua Rais Donald Trump kuwa ni mhalifu kutokana na ukiukaji wake wa mara kwa mara wa sheria za nchi."