Amnesty International yatoa tahadhari ya usalama kwa wageni wanaosafiri kwenda Marekani
Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International limetoa tahadhari ya usalama kwa raia wa nchi zote duniani wanaotaka kufanya safari nchini Marekani kufuatia matukio ya mauaji ya ufyatuaji risasi yaliyotokea katika majimbo ya Texas na Ohio.
Kwa mujibu wa gazeti la USA Today, shirika hilo la kutetea haki za binadamu limetoa indhari kwa raia wa nchi zote duniani kuhusu kufanya safari ya kutembelea Marekani na kuwataka wachukue tahadhari zinazohitajika na kuzingatia uwezekano wa kutokea hali ya hatari katika maeneo tofauti ya nchi hiyo wanayokusudia kuyatembelea.
Amnesty International vile vile limewataka wasafiri wanaoelekea nchini Marekani wajiepushe na kutembelea maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama sehemu za ibada, mashule na, klabu za usiku ambazo zililengwa katika mashambulio ya hivi karibuni.
Makundi mengine kadhaa ya kutetea haki za binadamu nayo pia yametoa tahadhari kuhusiana na kuongezeka matukio ya ukatili wa kutumia silaha nchini Marekani; na sambamba na Amnesty International yameyataja matukio ya ufyatuaji risasi yaliyotokea wiki hii nchini Marekani na kusababisha vifo vya makumi ya watu kuwa ni "Hali Mbaya ya Haki za Binadamu".

Venezuela na Uruguay tayari zimetoa tahadhari kama hiyo kwa raia wao wanaokusudia kufanya safari nchini Marekani au walioko safarini nchini humo hivi sasa.
Watu zaidi ya 80 waliuawa na kujeruhiwa katika matukio ya ufyatuaji risasi yaliyotokea tarehe 3 na 4 za mwezi huu wa Agosti katika miji ya Al Paso, Dayton na Chicago.
Kufuatia matukio hayo, asilimia 67 ya raia wa Marekani wametaka upitishwe muswada wa kuchunguza rekodi za wanunuzi wa silaha.
Maelfu ya watu huuawa na kujeruhiwa kila mwaka nchini Marekani katika matukio mbali mbali ya ufyatuaji risasi yanayotokea katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo.../