Julie Pace: Trump ana historia ndefu ya kueneza uongo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i55374-julie_pace_trump_ana_historia_ndefu_ya_kueneza_uongo
Mkuu wa ofisi ya shirika la habari la Associated Press mjini Washington amesema kuwa Rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump ana historia ndefe ya kueneza uongo na kutoa matamshi yasiyo sahihi wala yasiyo na msingi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 14, 2019 06:40 UTC
  • Julie Pace: Trump ana historia ndefu ya kueneza uongo

Mkuu wa ofisi ya shirika la habari la Associated Press mjini Washington amesema kuwa Rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump ana historia ndefe ya kueneza uongo na kutoa matamshi yasiyo sahihi wala yasiyo na msingi.

Julie Pace ameliambia shirika hilo la habari la Marekani kwamba, Donald Trump ndiye aliyekuwa msingi na chanzo cha kuenezwa habari ya uongo iliyodai kuwa: "Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani, si raia wa nchi hiyo na alizaliwa nje ya Marekani." 

Julie Pace ameongeza kuwa, Trump daima hutumia njama kama hizo kujitia motisha na nguvu mpya. 

Mkuu wa ofisi ya wa shirika la habari la Associated Press mjini Washington amesema kuwa, Trump hueneza habari kama hizo za uongo kwa muundo wa swali au kwa sura isiyoeleweka vyema na kujiachia fursa ya kuikadhibisha baadaye (pale anapabanwa na kuandamwa). 

Julie Pace: Trump ana historia ya kueneza habari za uongo

Siku chache zilizopita Rais Donald Trump wa Marekani alisambaza tena ujumbe wa Twitter ulioandikwa na mhafidhina Terrance Williams kuhusiana na kashfa na kifo cha bilionea Jeffrey Epstein.

Katika ujumbe huo Wlliams alidai kuwa rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton na mke wake Hillary aliyegombea urais dhidi ya Trump mwaka 2016 wanahusika na kifo cha bilionea Jeffrey Epstein aliyekuwa jela baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuhusika na genge la kuwauza watoto wadogo wanaotumikishwa kama watumwa wa ngono. Jeffrey Epstein alikuwa mfadhili na rafiki mkubwa wa Rais Donald Trump. 

Siku chache zilizopita Jeffrey Epstein alikutwa akining'inia katika jela ya Marekani wakati alipokuwa akisubiri kesi yake mahakamani kwa tuhuma za kufanya magendo ya watoto na wasichana wanaotumiwa katika utumwa wa ngono. 

Hadi sasa vyombo vya sheria vya Marekani havijathibitisha iwapo bilionea huyo rafiki mkubwa wa Trump alijinyonga au la, lakini maofisa wa serikali ya Marekani wanasema alijitia kitanzi yeye mwenyewe.