Independent: India inafanya mikakati ya kuwapokonya uraia mamilioni ya Waislamu
Gazeti la Independent linalochapishwa nchini Uingereza limefichua kwamba, serikali ya India inapanga mikakati ya kuwapokonya uraia watu wasiopungua milioni nne aghlabu yao wakiwa ni Waislamu na kuwatambua kuwa ni wahajiri wa kigeni.
Mikakati hiyo inafanyika katika fremu ya mipango ya chama tawala cha BJP chenye siasa kali za utaifa wa Kihindu.
Gazeti hilo limeripoti kuwa, serikali ya India imeanzisha kampeni ya kuwasaka na kuwatia nguvuni wale wanaodaiwa kuwa ni wahajiri haramu katika jimbo la milimani na maskini la Asam lilikolo katika mpaka wa nchi hiyo na nchi za Bangladesh na Myanmar. Jimbo hilo lina wakazi wanaokadiriwa kuwa milioni 33.
Ripoti ya independent inasema: Aghlabu ya wakazi wa eneo hilo ambao New Delhi inawatambua kuwa ni wahajiri wa kigeni, walizaliwa India na wana haki kamili za kiraia ikiwa ni pamoja na haki ya kupiga kura katika chaguzi mbalimbali.
Hadi sasa mamia ya raia wa eneo hilo wametiwa nguvuni kwa tuhuma za kuwa wahajiri wa kigeni na baadhi yao walikuwa wapiganaji wa zamani katika jeshi la India. Ripoti ya Independent inasema serikali ya New Delhi inapanga kujenga kambi makhsusi za kuwahifadhi raia hao Waislamu wanaonyang'anywa uraia.
Gazeti hilo la Uingereza limeongeza kuwa, serikali ya Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi inaendelea kutekeleza mipango yake licha ya tahadhari iliyotolewa na wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu na wanasheria wakisema kuwa hatua hiyo yumkini ikawalazimia makumi ya watu kujiua kwa kuhofia kukamatwa na kunyang'anywa uraia.
Mapema mwezi wa Sita mwaka huu Waziri Mkuu wa India alimteua mkuu wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) Amit Shah aliyewataja Waislamu kuwa ni "mchwa mweupe", kuwa Waziri wake wa mambo ya Ndani.
Gazeti la Times la Uingereza linasema kuwa Amit Shah ndiyo mhandisi wa siasa kuu za serikali ya New Delhi na mshauri mkuu wa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi.