UN: Waislamu wa Rohingya walioko Bangladesh hawataki kurejea Myanmar
Maafisa wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) na wale wa serikali ya Bangladesh wametangaza kuwa, Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbilia nchini Bangladesh hawataki kurejea katika nchi yao ya Myanmar.
Taarifa ya maafisa hao inasema kuwa, ni wakimbizi wachache mno wa Kirohingya walioko nchini Bangladesh ambao wamesema wako tayari kurejea nchini kwao. Abul Kalam, Kamishna wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa nchini Bangladesh amesema kuwa, ni familia 21 tu kati ya 1,056 ambazo zimesema ziko tayari kuwa sehemu ya mpango wa kuwarejesha wakimbizi Waislamu wa Rohingya walioko Bangladesh ambao ulipangwa kuanza kutekelezwa Alkhamisi ya kesho.
Afisa huyo wa UNHCR nchini Bangladesh anaeleza kwamba, asilimia kubwa ya wakimbizi hao wamesema hawataki kurejea nchini Myanmar.
Novemba mwaka 2017 Myanmar na Bangladesh zilikubaliana juu ya suala la kurejeshwa nyumbani mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Rohingya lakini hadi sasa si tu kwamba mwenendo wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi zaidi ya laki saba walioko Bangladesh haujaanza lakini pia wakimbizi hao wenyewe hawana hamu ya kurejea makwao kutokana na ukatili unaoendelea kufanywa na Mabudha wenye misimamo mikali nchini kwao wakishirikiana na jeshi.
Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka 2017.
Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea zaidi ya Warohingya milioni moja kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ikiwemo Bangladesh.