Nchi za Ulaya zaanza kuchunguza hatua za kupambana na Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i55550-nchi_za_ulaya_zaanza_kuchunguza_hatua_za_kupambana_na_trump
Umoja wa Ulaya umeanza kujadili mpango wa kupambana na rais wa Marekani, Donald Trump anayeendesha siasa chafu za kibiashara dhidi ya nchi za Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 23, 2019 03:14 UTC
  • Nchi za Ulaya zaanza kuchunguza hatua za kupambana na Trump

Umoja wa Ulaya umeanza kujadili mpango wa kupambana na rais wa Marekani, Donald Trump anayeendesha siasa chafu za kibiashara dhidi ya nchi za Ulaya.

Mpango huo wa kurasa 173 umewasilishwa kwa Kamisheni ya Ulaya. Baada ya kuwasilishwa, mkuu wa kamisheni hiyo, Ursula von der Leyen ametaka kuanzishwe mfumo maalumu wa nchi za Ulaya wa uwekezaji wa dola bilioni 100 kupitia kununua hisa katika mashirika makubwa ya bara hilo.

Lengo la mpango huo ni kupambana na siasa chafu za kibiashara za rais wa Marekani na kuandaa mazingira ya kuweza mashirika ya Ulaya kukabiliana vilivyo na mashirika makubwa ya mawasiliano ya Marekani kama Google, Apple, Amazon, Microsoft na Facebook.

Umoja wa Ulaya

 

Viongozi hao wa Ulaya wameitaka pia Kamisheni ya Ulaya kuwa na nguvu zaidi za utendaji za kuweza kupambana vilivyo katika vita vya kibiashara vilivyoanzishwa na Donald Trump dhidi ya nchi za Ulaya. Viongozi wa bara hilo wanaamini kuwa, kuna haja kwa nchi za bara hilo kuchukua hatua za kujibu uchokozi wa rais wa Marekani wa kuzipandishia ushuru bidhaa za Ulaya.

Itakumbukwa kuwa Donald Trump anatumia mbinu za kuzibana kiushuru bidhaa za feleji na aluminium zinazotoka barani Ulaya.

Kabla ya hapo pia Umoja wa Ulaya ulikuwa umetangaza kuwa, utachukua hatua madhubuti za kukabiliana na vitendo visivyo vya kiungwana vya rais wa Marekani katika masuala ya biashara.