Zarif: Marekani haihitaji adui ikiwa na rafiki kama Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i55991-zarif_marekani_haihitaji_adui_ikiwa_na_rafiki_kama_israel
Huku kukiwa na ripoti kuwa utawala haramu wa Israel umeweka vifaa vya ujasusi karibu na Ikulu ya White House, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amewakejeli wakuu wa Washington na kusema, Marekani ikiwa na muitifaki ambaye anafanya ujasusi dhidi yake basi haihitaji maadui.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Sep 13, 2019 23:11 UTC
  • Zarif: Marekani haihitaji adui ikiwa na rafiki kama Israel

Huku kukiwa na ripoti kuwa utawala haramu wa Israel umeweka vifaa vya ujasusi karibu na Ikulu ya White House, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amewakejeli wakuu wa Washington na kusema, Marekani ikiwa na muitifaki ambaye anafanya ujasusi dhidi yake basi haihitaji maadui.

Katika ujumbe wa kinaya kupitia ukurasa wake wa Twitter Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif, ameandika: "Timu B yashambulia Tena", akitumia istilahi ambayo ameibuni kuashiria kundi la kimataifa la wapenda vita linalomjumuisha waziri mkuu wa utawala wa Israel Benjamin Netanyahu.

Katika ujumbe wake, Zarif ameambatanisha ripoti ya jarida la Marekani la Politico ambalo limechapisha ripoti hiyo ya Israel kufanya ujasusi katika Ikulu ya Marekani. Katika ujumbe huo Zarif amemfahamisha Rais Trump wa Marekani kuwa, "ukiwa na rafiki wa karibu zaidi katika Timu B, ambaye anapora hazina za Marekani na kuteka sera za kigeni za Marekani kisha anamfanyia ujasusi Rais wa Marekani, basi Marekani haihitaji maadui."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran hapo alikuwa akimuashiria waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel baada ya jarida la Politico kuwanukuu maafisa watatu wa zamani wa serikali ya Marekani wakifichua kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umefunga vifaa vidogo vya ujasusi karibu na Ikulu ya White House na maeneo mengine muhimu mjini Washington D.C.

Kwa mujibu wa maafisa hao, moja ya vifaa hivyo vya kijasusi ni “StingRays” yenye uwezo wa kudukua mawasiliano ya simu. Duru za habari zinasema yumkini utawala haramu wa Israel ulipachika vifaa hivyo karibu na Ikulu ya White House katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ili ufuatilie mawasiliano ya simu ya Rais Donald Trump. Kufuatia taarifa hizo, Trump ambaye anajinadi kuwa rais aliye karibu zaidi na Israel katika historia ya Marekna, amewaambia waandishi habari kuwa, itakuwa vigumu kuamini kuwa Israel imejaribu kumfanyia ujasusi. Hata hivyo amesema kila kitu kinawezekana.