Trump akiri: Marekani inaingilia chaguzi zinazofanyika katika nchi nyingine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56299-trump_akiri_marekani_inaingilia_chaguzi_zinazofanyika_katika_nchi_nyingine
Katika kipindi cha Vita Baridi (Cold War) na baada ya vita hivyo Marekani ilikuwa ikitekeleza sera za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Moja ya mambo muhimu yanayodhihirisha ukweli huo ni mienendo ya Marekani ya kuingilia chaguzi katika nchi mbalimbali kwa lengo la kuwaingiza madarakani viongozi vibaraka na wanaofuata siasa za Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 28, 2019 22:57 UTC
  • Trump akiri: Marekani inaingilia chaguzi zinazofanyika katika nchi nyingine

Katika kipindi cha Vita Baridi (Cold War) na baada ya vita hivyo Marekani ilikuwa ikitekeleza sera za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Moja ya mambo muhimu yanayodhihirisha ukweli huo ni mienendo ya Marekani ya kuingilia chaguzi katika nchi mbalimbali kwa lengo la kuwaingiza madarakani viongozi vibaraka na wanaofuata siasa za Marekani.

Hivi sasa imebainika kwamba, Rais Donald Trump wa nchi hiyo amekiri suala hilo katika mazungumzo kati yake na viongozi wa ngazi ya juu wa Russia. Gazeti la Washington Post linalochapishwa nchini Marekani limetangaza kupitia ripoti yake ya mapema jana Jumamosi kuwa, mwaka juzi wa 2017 Trump aliwaambia viongozi wa Russia kwamba, hana wasiwasi juu ya uingiliaji wa Russia katika uchaguzi wa nchi yake wa mwaka 2016. Washington Post limeandika kuwa: Trump alibainisha haya katika mazungumzo aliyofanya White House na Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na Sergey Kislyak balozi wa wakati huo wa Russia mjini Washington. Trump alisema kuwa, Marekani pia inafanya hivyo hivyo kwa nchi nyingine. 

Trump, Lavrov na Kislyak walipokutana White House mwaka 2017 
 

Kukiri Trump kwamba marekani imekuwa ikiingilia chaguzi za nchi nyingine duniani kunadhihirisha masuala kadhaa. La kwanza ni kwamba, Washington inatumia sera za undumakuwili katika uwanja huu. Kwa maneno mengine ni kuwa, pale Marekani inapoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine jambo hili si fedheha kwa mtazamo wa viongozi wa Washington, bali pia linahesbiwa kuwa ni jambo jema na la kupongezwa linalofanyika eti kama ajili ya kuimarisha uhuru na demokrasia duniani! Wakati huo huo iwapo nchi yoyote itaingilia uchaguzi wa Marekani, viongozi wa nchi hiyo huiona hatua hiyo kuwa ni dhambi isiyosameheka  inayohatarisha usalama wa taifa wa nchi hiyo na wanakabiliana vikali na jambo hilo. Kadhia hii inadhihirika wazi zaidi katika tuhuma kwamba, Russia iliingia uchaguzi wa Rais Marekani mwaka 2016. Taasisi za kiintelijinsia za Marekani pia zinadai kuwa, Russia iliingia uchaguzi wa Marekani na kumsaidia Trump katika uchaguzi huo. Russia imepinga madai hayo na kusema kuwa haijaingilia uchaguzi huo wa rais wa Marekani. Robert Muller mchunguzi maalumu wa faili hilo amekamilisha uchunguzi wake baada ya miaka miwili na kuwasilisha matokeo yake kwa Wizara ya Sheria ya Marekani. Muller ameweka wazi katika ripoti hiyo kwamba, hakuna ushahidi wowote wenye mashiko wa kuthibiti kuwepo ushirikiano wa siri kati ya Trump na Russia.  

Hii ni katika hali ambayo, kuna vielelezo vingi vya uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi nyingine ikiwemo katika chaguzi za nchi mbalimbali Russia. Japokuwa viongozi wa Marekani wameibua makelele mengi na kuituhumu Russia  kuwa iliingia uchaguzi wa rais wa nchi hiyo lakini ukweli wa mambo ni kuwa, katika miaka ya karibuni hasa baada ya Vladimir Putin kuwa Rais wa Russia mwaka 2000, Washington iliingilia moja kwa moja na waziwazi katika chaguzi za Russia ukiwemo wa Bunge na Rais kupitia propaganda kubwa na vilevile kwa kuzitumia jumuiya za kiraia  eti za kutetea demokrasia. Washington ilifanya hivyo lengo likiwa ni kuwaingiza madarakani nchini Russia viongozi vibaraka wa Magharibi na wale wanaokwenda sambamba na siasa za Marekani, na wakati huo huo kufanya njama za kuzusha mivutano na kuzidisha maandamano ya wananchi dhidi ya Putin. Uingiliaji kati wa karibuni kabisa wa Marekani nchini Russia ulishuhudiwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu pale ubalozi wa Marekani mjini Moscow ulipochochea maandamano dhidi ya serikali.

Rais Vladimir Putin wa Russia
 

Andrey Klimov mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kulinda Mamlaka ya Russia katika Bunge la nchi hiyo amesema kuwa alama za uingiliaji kati wa nchi ajinabi zimeshuhudiwa katika  maandamano ya wiki kadhaa mjini Moscow. Klimov amesema: "Awali tulieleza kwamba Marekani na waitifaki wake wanafanya jitihada kutumia uchaguzi wa serikali za mitaa mjini Moscow kama wenzo wa kuwachochea wananchi na kuvuruga uchaguzi huo. Kwa bahati mbaya yale tuliyokuwa tukiyafikiria yamekuwa kweli."   

Mienendo inayofanana na hii ya Marekani imeshuhudiwa pia kwa nchi zinazopinga sera za kibeberu na kujitanua kwa serikali ya Washington kama Iran na Venezuela. Marekani imekuwa ikiingilia moja kwa moja masuala ya uchaguzi ya nchi hizo ili kufanikisha maslahi na malengo yake haramu.