Jimmy Carter aunga mkono mchakato wa kumuuzulu Trump
-
Jimmy Carter
Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy carter ambaye awali alikuwa mpinzani wa zoezi la aina yoyote la kumsaili na kumuuzu rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump, amejiunga na kambi inayotaka kuanzishwa zoezi la kumuuzulu kiongozi huyo.
Jimmy Carter amewaambia waandishi wa habari kwamba, anafuraha kubwa kuona Spika wa Kongresi ya Marekani Nancy Pelosi akishughulikia faili la kumsaili na kumuuzulu Donald Trump.
Carter amesisitiza kuwa, iwapo kura ya kumtimua Trump itapasishwa katika Kongresi ya Marekani, muswada huo utatumwa katika Baraza la Seneti ambako kutakuwepo udharura wa kupambana ipasavyo na maseneta wa chama cha Republican.
Rais Donald Trump wa Marekani anafuatiliwa sana baada ya kufichuliwa kuwa, katika mazungumzo yake na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine Julai 25 mwaka huu, alimshinikiza kiongozi huyo afanye uchunguzi wa kumfuatilia kisheria Hunter Biden, mwana wa kiume wa Joe Biden, anayetegemewa kuwa mshindani wake mkuu katika uchaguzi ujao wa rais wa Marekani, kama sharti la kuidhinisha msaada wa fedha wa masuala ya kijeshi kwa ajili ya Ukraine.
Baada ya kufichuliwa kashfa hiyo, Baraza la Wawakilishi la Marekani lilianzisha rasmi mchakato wa kumuuzulu Trump.