Polisi ya Marekani yaendeleza ukatili dhidi ya Wamarekani weusi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56612-polisi_ya_marekani_yaendeleza_ukatili_dhidi_ya_wamarekani_weusi
Katika kile kinachoonekana ni muendelezo wa mauaji ya kibaguzi yanayofanywa na askari polisi wa Marekani dhidi ya raia wa nchi hiyo wenye asili ya Afrika, mwanamke mweusi nchini humo ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi kupitia dirisha la chumbani kwake mapema Jumamosi
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Oct 14, 2019 04:49 UTC
  • Polisi ya Marekani yaendeleza ukatili dhidi ya Wamarekani weusi

Katika kile kinachoonekana ni muendelezo wa mauaji ya kibaguzi yanayofanywa na askari polisi wa Marekani dhidi ya raia wa nchi hiyo wenye asili ya Afrika, mwanamke mweusi nchini humo ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi kupitia dirisha la chumbani kwake mapema Jumamosi

Atatiana Jefferson, mwenye umri wa miaka 28, amekuwa akiishi katika makazi ya Fort Worth, mjini Texas na mpwa wake mwenye umri wa miaka minane. Jirani yake aliwapigia simu polisi wakidai kuwa wana wasiwasi kwa kuwa mlango wa mbele ya nyumba ya mwanamke huyo ulikuwa wazi usiku wa kuamkia jana. Hapo ndipo afisa mmoja alimpiga risasi mwanamke huyo na kumuua akiwa chumbani kwake.

Mapema mwezi Agosti mwaka huu, moto wa hasira ulizuka katika pembe mbalimbali za Marekani baada ya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii picha iliyowaonyesha askari polisi wawili waliopanda farasi wakimpeleka kituoni katika mji wa Galveston jimboni Texas raia mweusi, huku wakiwa wamemfunga kamba.

Polisi ya Marekani imekuwa ikiwaua raia weusi hata wanaojisalimisha

Kitendo hicho kilikumbusha historia ndefu ya ukatili, utumwa na ubaguzi wa rangi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika, katika enzi za utenganishaji jamii za watu wa nchi hiyo.

Hivi karibuni, wanasheria na familia ya kijana mwenye asili ya Kiafrika aliyeuawa na polisi mzungu nchini Marekani walifanya maandamano mbele ya mahakama wakilaani kitendo cha kufutiwa mashtaka polisi huyo muuaji katika jimbo la Pennsylvania.

Mienendo hiyo isiyo ya kiuadilifu ya polisi na vyombo vya mahkama nchini Marekani dhidi ya jamii ya Wamarekani weusi, imekuwa ikilalamikiwa vikali katika maeneo tofauti ya nchi hiyo inayojidai kuwa mtetezi wa haki za binaadamu duniani.