China yaitahadharisha Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani ya Hong Kong
Serikali ya China imeendelea kulaani vikali uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya mji wa Hong Kong, kwa kupasisha muswada uliopewa jina la 'Haki za binaadamu na demokrasia.'
Yang Guang, Msemaji wa Ofisi ya Masuala ya Hong Kong na Macao katika baraza la mawaziri la China amewaambia waandishi wa habari mjini Beijing, kwamba kupasishwa muswada huo na Marekani, ni hatua ya kijeuri na ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Aidha Guang ameitaja hatua hiyo ya Washington kuwa ni ya kichokozi na yenye lengo la kuwachochea waandamanaji katika eneo hilo. Msemaji wa Ofisi ya Masuala ya eneo la Hong Kong amesema kuwa, iwapo muswada huo utapitishwa rasmi kuwa sheria, utadhoofisha uhusiano wa Beijing na Washington kama ambavyo pia utayadhuru maslahi ya Marekani.
Afisa huyo wa serikali ya China amezidi kubainisha kwamba kupasishwa muswada huo kunabainisha siasa ghalati na za undumakuwili za Marekani na pia kujigamba bure baadhi ya viongozi wa Washington kuhusiana na suala la haki za binaadamu na demokrasia. Itakumbukwa kuwa Jumanne iliyopita Congress ya Marekani ilipasisha muswada uliopewa jina la 'muswada wa haki za binaadamu na demokrasia mwaka 2019 kwa ajili ya Hong Kong.' Kabla ya hapo pia Eliot Engel mkuu wa kamisheni ya masuala ya kigeni na Michael McCann mbunge wa congress hiyo walinukuliwa wakiwaunga mkono waandamanaji wa Hong Kong na kuwataka waendeleze maandamano hayo.