Rais Tayyip Erdoğan: Uturuki haiogopi vikwazo vya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56679-rais_tayyip_erdoğan_uturuki_haiogopi_vikwazo_vya_marekani
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amedai kwamba lengo la operesheni za nchi yake kaskazini mwa Syria lipo wazi na kwamba serikali ya Ankara haiogopi hata kidogo vikwazo vya Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 17, 2019 09:52 UTC
  • Rais Tayyip Erdoğan: Uturuki haiogopi vikwazo vya Marekani

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amedai kwamba lengo la operesheni za nchi yake kaskazini mwa Syria lipo wazi na kwamba serikali ya Ankara haiogopi hata kidogo vikwazo vya Marekani.

Rais Erdoğan ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari mjini Ankara na kuongeza kuwa, Wamarekani wanaiwekea mashinikizo Uturuki kwa lengo la kuifanya isitishe operesheni zake  nchini Syria, lakini lengo la nchi yake katika vita hivyo liko wazi hivyo haina hofu yoyote na vikwazo hivyo. Rais Recep Tayyip Erdoğan ameongeza kwamba, kamwe serikali ya Ankara haiwezi kusitisha vita na kuingia katika mazungumzo na kundi inalolichukulia kuwa la kigaidi. Amesema, makundi yanayobeba silaha ni lazima yarejee nyuma kutoka mipaka ya Uturuki hadi umbali wa kilometa 32 ndani ya ardhi ya Syria.

Jeshi la Uturuki likiwa katika maeneo ya kaskazini mwa Syria

Operesheni za kijeshi za Uturuki huko kaskazini mwa Syria zilizopewa jina la 'Chemchemi ya Amani' zilianza siku ya Jumatano ya tarehe 9 Oktoba kwa lengo la kukabiliana na ugaidi na kusafisha mipaka ya Uturuki na Syria kutokana na uwepo wa wanamgambo wa Kikurdi ambao wanatambuliwa na serikali ya Ankara kuwa magaidi. Operesheni hizo zimekosolewa vikali na jamii ya kimataifa na hasa raia na serikali ya Syria. Katika uwanja huo Jumatatu ya tarehe 14 Oktoba Trump alitoa taarifa ya kuiwekea vikwazo vipya serikali ya Uturuki. Vikwazo hivyo vinawalenga viongozi wa sasa na wa zamani wa serikali ya Ankara pamoja na shakhsia ambao wanatuhumiwa kuhusika na machafuko kaskazini mwa Syria. Vikwazo hivyo pia vimezihusisha Wizara za Ulinzi na Nishati pamoja na mawaziri watatu wa Uturuki.