Oct 24, 2019 06:17 UTC
  • UN yawataka Wazayuni waache kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina

Ripota wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameitaka jamii ya kimataifa isiendelee kukaa kimya bali iuchukulie hatua utawala dhalimu wa Israel na kuulazimisha uache kuzikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Michael Lynk amewasilisha ripoti yake mapema leo Alkhamisi mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, Israel inaendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina, hivyo jamii ya Kimataifa inapaswa kuuchukulia hatua kali zaidi utawala wa Kizayuni wa Israel.

Amesema, jamii ya kimataifa imetoa maazimio na taarifa chungu nzima za kuilaani Israel kwa kuendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina lakini maazimio na matamko yote hayo yameshindwa kutekelezwa kivitendo.

Israel inapora ardhi za Wapalestina na kubomoa nyumba zao na halafu kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

 

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, Israel inatumia vibaya udhaifu wa maamuzi ya kisiasa wa jamii ya kimataifa hususan nchi za Magharibi na za viwanda.

Ripota huyo wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu vile vile ameitaka jamii ya kimataifa kulizingatia sana suala la kuzidi kuporwa ardhi za Wapalestina pamoja na kuvunjiwa nyumba zao na mahala pake kujengwa vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni huko Ukingo wa Magharibi wa Mtro Jordan na Quds Mashariki.

Tarehe 23 Disemba 2016, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nabari 2334 linaloutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uache mara moja na kikamilifu ujenzi wake wote wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina. Hata hivyo azimio hilo na mengineyo mengi yamebakia vivi hivi bila ya kutekelezwa kivitendo.

Tags