HAMAS yaitaka jamii ya kimataifa kuwasaidia watu wa Gaza
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa mwito wa kupitishwa maamuzi ya dharura na jamii ya kimataifa ya kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kuwasaidia wananchi wa ukanda huo wanaokabiliwa na masaibu mengi.
Taarifa ya HAMAS imesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni unatoa adhabu za kikatili zaidi za umati dhidi ya raia wasio na hatia wa Palestina kupitia mzingiro wa Ukanda wa Ghaza na kufunga vivuko.
Harakati ya HAMAS imesisitiza katika taarifa yake hiyo kwamba, utawala wa Kizayuni unaendeleza vita vya jinai vya kuwafanya wakazi wa Gaza kubakia na njaa huku hali mbaya ya kibinadamu na ukosefu wa huduuma muhimu katika Ukanda wa Gaza ikizidi kuwa mbaya siku baada ya siku.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeonya kuwa, takriban watoto 3,000 wa Kipalestina wapo katika ncha ya kuaga dunia mbele ya jamaa zao kwa kukosa matibabu ya utapiamlo wa kiwango cha juu kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Hayo yanajiri huku Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu akitangaza kuwa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni tangu tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Ukanda wa Gaza, yameligeuza eneo hilo linalokabiliwa na changamoto nyingi kama umasikini na ukosefu wa huduma muhimu, kuwa Jahanamu ya duniani.