Marekani na magendo ya mafuta ya Syria
Jumatatu iliyopita Mark Esper, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alidai kuwa eti nchi yake ipo nchini Syria kwa ajili ya kulinda vyanzo vya mafuta vya taifa hilo la Kiarabu, na kwamba Washington haitaki kuona vyanzo hivyo vikiingia kwa mara nyingine katika udhibiti wa kundi la Daesh (ISIS).
Ni vyema kukumbusha kwamba tangu mwaka 2011 Syria imekuwa katika vita dhidi ya magaidi wanaotoka nchi tofauti. Mbali na hayo, serikali ya Syria imekuwa chini ya mashinikizo makali ya kigeni hususan kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya. Moja ya sekta muhimu ambazo zimelengwa ili kuiwekea mashinikizo serikali ya Syria, ni kufunga vyanzo vya kifedha vya nchi hiyo hususan mapato ya mafuta. Katika uwanja huo, Marekani na Umoja wa Ulaya, zimeiwekea vikwazo Syria na sekta yake ya mafuta, ili kuinyima Damascus mapato ya fedha. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mafuta ya Syria, kiwango cha uzalishaji mafuta kabla ya kuanza vita ndani ya nchi hiyo hapo mwaka 2011, kilikuwa ni mapipa laki tatu na elfu 85 kwa siku, ambapo mapipa laki moja na elfu 50 yalikuwa yakiuzwa nje ya nchi, huku yaliyobakia yakitumika ndani ya nchi. Hata hivyo taathira ya vikwazo vya Marekani na Ulaya imeisababishia hasara kubwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Katika uwanja huo, Meneja Mipango na Ushirikiano wa Kimataifa wa Wizara ya Mafuta na Madini ya Syria amesema kuwa, hasara ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja tangu kuanza mgogoro wa ndani kuanzia mwaka 2011 hadi Julai 2019 iliyoilenga Wizara ya Mafuta ya nchi hiyo pamoja na mashirika yaliyo chini ya wizara hiyo, imefikia karibu dola bilioni 82, ikijumuisha karibu dola bilioni 17 za hasara ya moja kwa moja na bilioni 65, ambayo ni hasara isiyo ya moja kwa moja. Katika hatua ya mwanzo, Marekani na Umoja wa Ulaya zinakusudia kuizuia serikali ya Damascus kunufaika na mapato yake yanayotokana na mafuta. Na hatua ya pili ambayo inatekelezwa tu na serikali ya Marekani, ni kudhibiti yenyewe vyanzo vya mafuta ya nchi hiyo ya Kiarabu. Hii ni kusema kuwa, Marekani ambayo imeiwekea vikwazo sekta ya mafuta ya Syria, imekuwa ikifanya magendo ya mafuta ya nchi hiyo hususan katika jimbo la Deir Ez-Zor. Kuhusiana na suala hilo, Igor Konashenkov, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia amesema kuwa taasisi za serikali ya Marekani, zinahusika katika magendo ya mafuta ya Syria ambapo kwa mwezi mmoja zinaingiza zaidi ya dola milioni 30 kutokana na magendo ya nishati hiyo muhimu ya Syria.

Hata kama Rais Donald Trump wa Marekani anadai kuwa eti nchi yake inayalinda mafuta ya Syria kwa lengo la kuzuia yasiangukie mikononi mwa kundi la Daesh (ISIS), lakini Benjamin Hart, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, ameandika katika makala yaliyochapishwa na jarida la New York kwamba: "Kipaumbele cha kwanza katika siasa za Trump nchini Syria, ni kupora na kudhibiti vyanzo vya mafuta vya nchi hiyo ya Kiarabu." Mtazamo huo wa siasa za Trump kuhusu mafuta ya Syria, umekuja katika hali ambayo vyanzo vya mafuta vya nchi hiyo, ni mali halali ya serikali ya Damascus, hivyo Washington haina haki yoyote ya kuchukua maamuzi kuhusiana na suala hilo. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Igor Konashenkov, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia akasema kuwa: "Kile ambacho Washington inakifanya nchini Syria ni kudhibiti moja kwa moja visima vya mafuta vya upande wa mashariki mwa nchi hiyo, ambapo kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa, shughuli za Washington katika uwanja huo ni kinyume cha sheria na misingi ya kimataifa." Ukweli ni kwamba, Marekani ambayo imeiwekea Syria vikwazo kwenye mapato yake, hivi sasa inatekeleza uharamia wa kimataifa wa moja kwa moja kupitia magendo ya mafuta ya nchi hiyo.