Trump akosoa matamshi ya Macron kuhusu Nato
Rais wa Marekani ameyataja matamshi ya Rais mwenzake wa Ufaransa kuhusu Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) kuwa yaliyotiwa chumvi.
Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa kile alichozungumza Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuhusu Nato kimetiwa chumvi na ni aina fulani ya mashambulizi. Rais Trump ameyasema hayo katika mazungumzo na Jens Stoltenberg Katibu Mkuu wa Muungano wa Nato mjini London Uingereza.
Trump ameyasema hayo baada ya hivi karibuni Rais Macron wa Ufaransa kusema kuwa muungano wa Nato umekufa ubongo. Trump aidha amebainisha kuwa Marekani inanufaika kwa kiwango kidogo sana na muungano huo wa kijeshi na ndiyo inayoisaidia Ulaya.
Kitambo Trump aliwahi kusema kuwa muungano wa Nato umepitwa na wakati.
Akiendelea na mazungumzo yake na Jens Stoltenberg, Rais wa Marekani amekariri matamshi yake ya kuidhalilisha Saudi Arabia na kuongeza kuwa: Marekani ina uhusiano mzuri na Saudia na kwamba wanajeshi kadhaa wa nchi hiyo wamepelekwa Saudi Arabia; na kuwa Wasaudia wanaipatia Washington mamilioni ya dola. Rais wa Marekani ameongeza kuwa Umoja wa Ulaya unaamiliana na Washington kusiko na uadilifu mkubwa kuhusu biashara.
Katika mazungumzo hayo huko London Trump kwa mara nyingine ameunga mkono kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya. Rais huyo wa Marekani leo Jumanne amewasili London kwa ajili ya kuhudhuria kikao cha viongozi wa Muungano wa Nato.