Mkasa wa moto kiwandani waua watu 43 nchini India
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57753-mkasa_wa_moto_kiwandani_waua_watu_43_nchini_india
Makumi ya watu wameuawa katika mkasa wa moto uliotokea katika jengo la ghorofa nne lenye kiwanda katika eneo la kaskazini la Filimistan huko New Delhi, mji mkuu wa India.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 08, 2019 08:31 UTC
  • Mkasa wa moto kiwandani waua watu 43 nchini India

Makumi ya watu wameuawa katika mkasa wa moto uliotokea katika jengo la ghorofa nne lenye kiwanda katika eneo la kaskazini la Filimistan huko New Delhi, mji mkuu wa India.

Monika Bhardwaj, Naibu Kamishna wa Polisi katika wilaya ya Kaskazini jijini New Delhi amesema, watu 43 wamepoteza maisha katika ajali hiyo, huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Amesema watu 16 wamelazwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya ya kuungua, na kwamba wengine 60 wameokolewa kutoka kwenye jengo hilo lililoteketea.

Kulingana na ripoti za wanahabari, alfajiri ya leo Jumapili mwendo wa saa kumi, moto ulitokea katika kiwanda cha mbao kwenye barabara ya Rani Jhansi, moja ya barabara kuu za New Delhi.

Gari la zima moto likielekea katika eneo la tukio

Akthari ya wazima moto walijaribu kufika katika eneo la tukio kujaribu kuuzima na kuudhibiti moto huo usienee katika majengo mengine, lakini walishindwa kutokana na wembamba wa barabara.

Februari mwaka huu, watu 17 waliaga dunia katika mkasa mwingine wa moto uliotokea katika jengo la ghorofa sita viungani mwa mji mkuu wa India, New Delhi.