Radiamali ya Marekani kwa maneva ya Iran, Russia na China
Sean Robertson msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) amesema kuwa nchi hiyo ina taarifa kuhusu maneva kati ya Iran, Russia na China na inafuatilia maneva hiyo.
Robertson amesisitiza kuwa eti Marekani, washirika na waitifaki wake wanaendeleza jitihada za kudhamini uhuru wa safari za meli na uhuru wa biahara katika maji ya kimataifa.
Wu Qian Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China juzi alisema kuwa lengo la maneva hiyo ya pamoja kati ya Iran, Russia na China katika bahari ya Oman ni kuanzisha uratibu kati ya askari jeshi wa majini wa nchi hizo tatu na kutuma ujumbe wa nia njema.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China ameongeza kuwa kikosi cha majini cha nchi hiyo kinashiriki katika maneva hiyo ya siku nne ikiwa na manowari ya Xining.
Wizara ya Ulinzi ya Russia pia imeeleza kuwa meli tatu za kikosi cha majini cha bahari ya Baltic cha Russia zitashiriki kwenye maneva hiyo ya pamoja ya baharini kati ya nchi hiyo, Iran na China.
Maneva ya kwanza ya baharini ya pande tatu za Iran, Russia na China inaanza leo Ijumaa katika fremu ya kuimarisha na kuzidisha usalama wa biashara za kimataifa kaskazini mwa bahari ya Hindi na katika bahari ya Oman.