Uamuzi wa Trump kumbadilisha Waziri wa Mambo ya Nje
Gazeti moja la Marekani limeeleza uwezekano wa kubadilishwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na kuteuliwa mtu mwingine mahala pake.
Gazeti hilo la Washington Post limeandika leo Ijumaa kwamba Trump anawatafuta watu wengine wanaofaa kushika nafasi hiyo ambayo kwa sasa inashikiliwa na Mike Pompeo. Jina ambalo linatajwa zaidi kuweza kuchukua nafasi hiyo ni la Robert O'Brien, ambaye kwa sasa ni Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani. Lingine ni la Steven Mnuchin, Waziri wa Fedha wa nchi hiyo.
Katika miezi ya karibuni kumekuwepo na tetesi kuwa huenda Pompeo akajiuzulu nafasi hiyo na kugombea useneta wa jimbo la Kansas. Hata hivyo gazeti hilo limeandika kuwa Pompeo mwenyewe amesema kuwa hana nia ya kugombea kiti hicho na kwamba watu wa karibu yake pia wanasema kuwa hajachukua uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo.
Baadhi ya vyombo vya kuaminika vimeliambia gazeti la Washington Post kwamba Mitch McConnell, Kiongozi wa Waliowengi katika Seneti ya Marekani anamshinikiza Pompeo aweze kugombea nafasi ya useneta katika jimbo hilo kwa sababu ana wasi wasi kwamba huenda kiti hicho kikachukuliwa na Kris Kobach, mgombea wa chama cha Democrat.
Rais wa Marekani amenukuliwa akisema kuwa iwapo nafasi hiyo itakabiliwa na hatari ya kuchukuliwa na Wademocrat, huenda Pompeo akabadili msimamo wake na kuchukua uamuzi wa kugombea kiti hicho.