Wanajeshi waliostaafu Marekani wahamia Vietnam kupata huduma bora za afya
Maelfu ya Wamarekani waliostaafu wakiwemo maveterani wa kivita wanaihama nchi yao na kuelekea Vietnam ili kupata huduma bora za afya na zenye bei nafuu.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Los Angeles Times la Marekani, idadi kubwa ya wanajeshi wa Marekani ambao wakati mmoja walipigana vita nchini Vietnam sasa wamerejea katika nchi hiyo ili kunufaika na huduma zake nzuri na zenye bei nafauu za Kiafya.
Ripoti hiyo imesema kuwa, wanajeshi zaidi ya 58,000 Wamarekani walifariki katika vita vya Vietnam na baada ya vita hivyo kumalizika mwaka 1975, sasa baadhi ya wanajeshi hao wanarejea katika nchi hiyo wakiomba msamaha na maelewano. Ripoti hiyo imesema wanajeshi hao wa Marekani hawarejei Vietnam kwa sababu hizo pekee bali sasa wengi wanafika katika nchi hiyo kutokana na bei nafuu ya nyumba, huduma za afya na kiwango kizuri cha maisha.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa mbali na Vietnam, idadi kubwa ya waliostaafu katika sekta ya umma Marekani pia wanahamia katika nchi kama vile Thailand, Ufilipino na Malaysia ili kukimbia umasikini katika nchi yao.
Hayo yanaripotiwa wakati ambao, takwimu za serikali ya Marekani zinaonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la visa vya kujiua wanajeshi waliostaafu nchini humo huku wengine wengi wakikumbwa na matatizo ya kiakili.
Utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani unadai kuwa, hali ya maveterani wa kivita nchini humo ni nzuri lakini ukweli wa mambo ni kinyume cha madai hayo.