Nchi Kadhaa Duniani zalaani mauaji ya Qassem Soleimani
Nchi kadhaa duniani zimeilaani vikali Marekani kwa kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Russia imesema kitendo hicho cha Marekani kitazidisha taharuki eneo la Asia Magharibi. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema Soleimani alikuwa analinda maslahi ya kitaifa ya Iran kwa kujitolea. Russia aidha imewatumia salamu za rambirambi watu wa Iran kufuatia kuuawa kamanda huyo wa ngazi za juu.
Waziri wa Masuala ya Ulaya nchini Ufaransa Amelie de Montchalin amesema hatua ya Marekani kumuua Meja Jenerali Suleimani itafanya dunia iwe sehemu hatari zaidi. Amesema Rais Emmanuel Macron atawasiliana hivi karibuni na viongozi wa eneo. China nayo imetoa taarifa ikiitaka Marekani iache kuchukua hatua ambazo zitavuruga zaidi utulivu wa kimataifa.
Naye kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Uingereza, chama cha Leba, Jeremy Corbyn ametoa wito kwa serikali ya Uingereza kuchukua hatua za kukabiliana na vitendo vya kichokozi vya Marekani.
Meja Jenerali Qassem Solaimani na naibu mkuu wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq, al Hasdul Shaabi, Abu Mahdi al Muhandes wameuawa shahidi mapema leo Ijumaa katika shambulizi la roketi lililofyatuliwa na helikopta ya Marekani katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani imetangaza kuwa, Rais Donald Trump wa nchi hiyo ametoa amri ya kuuliwa shahidi Jenerali Qassem Soleimani.