Afisa wa zamani wa White House: Trump ataifanya Iran ijitoe NPT
Afisa mmoja wa zamani wa Ikulu ya Marekani, White House ametahadharisha kwamba, siasa mbovu na ghalati za rais wa nchi hiyo Donald Trump zinaisukuma Iran kwenye kujitoa katika Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia, NPT.
Profesa Frank N. von Hippel, msaidizi wa zamani wa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa katika Ofisi ya Mipango ya Elimu na Teknolojia ya White House ameliambia shirika la habari la IRNA kwamba, kitendo cha Trump cha kuitoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni hatari sana na kusisitiza kwamba, kama siasa zinazokatisha tamaa za Umoja wa Ulaya hazitobadilika mbele ya mashinikizo ya Donald Trump, basi tutarajie kutokea mambo mabaya zaidi kama vile kujitoa Iran kwenye Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia, NPT.
Professa Hippel ameongeza kuwa, ni jambo lisilo na shaka kwamba kamwe Iran haitozipigia magoti Marekani na Umoja wa Ulaya bali itaendelea kusimama imara na itajibu kila hatua itakayochukuliwa dhidi yake.
Afisa huyo mwandamizi wa Ikulu ya Marekani wakati wa urais wa Bill Clinton vile vile amesema, siasa za nchi za Ulaya ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA baada ya Marekani kujitoa hazikubaliki, ni za kukatisha tamaa. Amesema si nchi za Ulaya tu, bali hata China na Russia nazo zimeshindwa kuchukua hatua za maana za kukabiliana na mashinikizo ya Marekani iliyoekewa Iran baada ya Trump kujitoa katika mapatano hayo.
Jana Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikosoa vikali hatua zilizo kinyume cha sheria za nchi za Ulaya kuhusu JCPOA na kusema kuwa, kama faili la Iran litarudishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, basi Tehran itafikiria kujitoa kwenye mkataba wa NPT.