WHO: Tusisahau Ebola wakati tunashughulikia Corona
https://parstoday.ir/sw/news/world-i59129-who_tusisahau_ebola_wakati_tunashughulikia_corona
Shirika la Afya Duniani WHO limesema dunia ni lazima iendelee kufadhili vita dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola kwani kuzembea katika hilo kutaleta madhara makubwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 13, 2020 11:52 UTC
  • WHO: Tusisahau Ebola wakati tunashughulikia Corona

Shirika la Afya Duniani WHO limesema dunia ni lazima iendelee kufadhili vita dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola kwani kuzembea katika hilo kutaleta madhara makubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ameashiria hali ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na kusema:"Ingawa dunia hivi sasa imejikita zaidi katika virusi vya Corona lakini hatuwezi na hatupaswi kusahau kuhusu Ebola.”

DRC inakabiliwa na mlipuko wa Ebola ambao ni wa pili kwa ukubwa duniani katika historia na ambao tayari umeshua watu 2,200 na visa 3,300 kuthibitishwa tangu ulipozuka na kutangazwa rasmi August Mosi 2018.

mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus

Mkuu huyo wa WHO amesema ametiwa moyo na mwenendo wa sasa ambapo kumekuwa na visa vitatu tu vya waathiriwa kwa wiki nzima iliyopita na hakujakuwa na kisa chochote katika siku tatu zilizopita. Dkt. Tedros ameonya kwamba hadi pale ambapo hatutakuwa na kisa chochote kwa siku 42, ugonjwa huu haujakwisha bado.

Ikumbukwe kuwa, mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa hatari wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika.