Kumalizika ziara ya Trump nchini India
https://parstoday.ir/sw/news/world-i59418-kumalizika_ziara_ya_trump_nchini_india
Ziara ya siku mbili ya Rais Donald Trump wa Marekani huko India imemalizika katika hali ambayo hakujatangazwa habari yoyote kuhusu kufikiwa mapatano makubwa ya kibiashara kati ya nchi mbili hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 27, 2020 04:38 UTC
  • Kumalizika ziara ya Trump nchini India

Ziara ya siku mbili ya Rais Donald Trump wa Marekani huko India imemalizika katika hali ambayo hakujatangazwa habari yoyote kuhusu kufikiwa mapatano makubwa ya kibiashara kati ya nchi mbili hizo.

Licha ya kusainiwa makubaliano ya silaha ya thamani ya dola bilioni tatu kati ya nchi mbili hizo ambayo Trump ameyazungumzia sana India kwa upande wake haijaweza kukidhi matarajio yake katika ziara hiyo ambayo imeigharimu pakubwa kwa kuwa mwenyeji wa Rais wa Marekani na ujumbe aliofuatana nao nchini humo. 

Trump akiwa na Waziri Mkuu wa India Narendara Modi mjini New Delhi

Awali kabla ya kuanza safari yake hiyo nchini India mbali na kukosoa uhusiano wa kibiashara kati ya nchi mbili Trump alikuwa ametaka kuangaliwa upya hali ya sasa ya uhusiano kati ya nchi mbili hizo. Rais wa Marekani siku kadhaa kabla ya kuanza siara yake hiyo huko India alieleza kutoridhishwa na  uhusiano wa kibiashara kati ya Washington na New Delhi na kudai kuwa India haikuwa ikiamiliana vizuri na Marekani. Akihutubia kwenye uwanja mkubwa wa mchezo wa kriketi wa Motera katika mji wa Ahmedabad India Trump licha ya yeye binafsi kuwa na uhusiano mzuri na Narendara Modi Waziri lakini alikosoa siasa za serikali ya Waziri Mkuu huyo na kusema kuwa anafanya juhudi ili kusainiwa makubaliano bora ya kibiashara katika siku zijazo kati ya Washington na New Delhi.   

Kabla ya hapo, viongozi wa ngazi ya juu wa India walieleza kuwa mazungumzo ya kibiashara kati ya nchi mbili hayakuwa na matunda kwa sababu Marekani iliwasilisha matakwa mengi. India ilisema kuwa ingeliafiki kuingizwa nchini bidhaa za maziwa kutoka Marekani hata hivyo Washington katika hatua zake za kutaka makuu ilitaka pia bidhaa nyingine za Marekani kama zile za chakula zifike kwenye masoko ya India.  

Serikali ya Trump imewasilisha maombi mengi ya kibiashara kwa India katika fremu ya hatua zake jumla za kibiashara yaani kuhakikisha kuwa inapata manufaa makubwa mkabala na kunufaika kidogo upande wa  pili; ikiwa ni pamoja na hatua yake ya kuishinikiza India ili iyaandalie mazingira mazuri makampuni ya Kimarekani yanayojihusisha na utoaji wa kadi za benki (credit Cards) hata hivyo India iliakhirisha mazungumzo kuhusiana na suala hilo kwa sababu Washington ilipinga ombi la New Delhi la kuzifanyia majaribio malighafi za vyakula kutoka Marekani. Kabla ya hili pia, India iliacha kuingiza nchini humo bidhaa za maziwa kutoka Marekani kwa sababu za kimadhehebu hatua ambayo haikuridhiwa na Marekani.  

Serikali ya Marekani haina mpango wa kufanya mazungumzo ya jadi na India hivi sasa ili kufikia mapatano makubwa katika nyuga mbalimbali. Ni dhahir shahir kwamba ziara ya Trump nchini India ambapo kuna uchaguzi mwaka huu huko Marekani imefanyika lengo likiwa ni kunufaika kipropaganda kwa kuzingatia alivyokaribishwa katika ziara yake hiyo na pia kusainiwa makubaliano ya silaha na baadhi ya mikataba katika nyanja za nishati na nyinginezo. Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alimuahidi Trump kuwa atalakiwa na mamilioni ya watu hata hivyo ni karibu watu laki moja tu ndio waliojitokeza kumkaribisha rais huyo wa Marekani.   

Rais wa Marekani na mkewe wakiwa pamoja na wenyeji wao Waziri Mkuu wa India na mkewe 

Tovuti ya habari ya Forbes imeandika katika ripoti yake kuwa: Ziara ya Trump nchini India inaweza kuwa na athari chanya kwa watu milioni nne na nusu waliotimiza masharti ya kupiga kura huko Marekani wawe ni Wahindi au Wamerekani wenye asili ya India.   

Trump amewavunja moyo wananchi wa India kuhusu kusainiwa makubaliano makubwa ya kibiashara kati ya India na Marekani licha ya makaribisho na pongezi nyingi za viongozi wa nchi mbili kuhusu uhusiano kati ya nchi mbili hizo. Kuhusu suala hilo Trump alisema: Sisi tutaainisha wakati mwingine wa kusaini makubaliano makubwa ya kibiashara na India. Huenda makubaliano hayo yakasainiwa kabla ya uchaguzi wa Rais wa Marekani mwezi Novemba mwaka 2020.   

Thamani ya biashara kati ya pande mbili za India na Marekani katika miezi 9 ya mwanzo wa mwaka uliopita wa 2019 ilikuwa karibu dola bilioni 110. Katika kipindi hicho thamani ya uuzaji nje bidhaa za Marekani huko India iliongezeka kwa asilimia 4 ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho cha mwaka wa kabla yake ambayo ilifikia dola bilioni 45.3. Wakati huo huo thamani ya uingizaji bidhaa nchini Marekani kutoka India inakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5 na kufikia dola bilioni 65.6. Akihutubia huko Ahmedabad Trump alidai kuwa katika serikali yake kiwango cha biashara kati ya nchi mbili kimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 40.   

Baraza la Ushirikiano wa Kistratejia kati ya India na Marekani linakadiria kuwa thamani ya biashara ya pande mbili za India na Marekani itafikia dola bilioni 238 kufikia mwaka 2025. 

Licha ya tabiri zote hizo, kuendelea hitilafu za kibiashara kati ya nchi mbili na kufeli mazungumzo ya pande hizo kuhusu suala hilo  kumempelekea Robert Lighthizer Mjumbe wa ngazi ya juu wa masuala ya kibiashara wa Marekani kufuta safari yake nchini India katikati ya mwezi huu wa Februari.  

Kusainiwa makubaliano makubwa ya kibiashara na India kuna umuhimu mkubwa sana kwa Trump kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais huko Marekani mwezi Novemba mwaka huu. Trump si tu anataka kuwaonyesha wananchi wa Marekani kuwa amepata mafanikio makubwa ya kicuhumi bali anataka kuwathibitishia waitifaki wake kwamba mtazamo wake mkali kuhusu masuala ya kibiashara umefanya mambo kuwa kwa maslahi ya Marekani. Pamoja na hayo inaonekana kuwa ni jambo lililo mbali kwamba New Delhi katika mazungumzo yajayo ya kibiashara kati yake na Washington itaipatia fursa kubwa serikali ya Trump.