Taleban: Madai kwamba tunakusudia kuvunja makubaliano si ya kweli
Msemaji wa Ofisi ya Kisiasa ya Kundi la Taleban ametupilia mbali ripoti za vyombo vya habari kwamba kundi hilo linakusudia kutofungamana na makubaliano yake na Marekani.
Suhail Shaheen ameyasema hayo katika taarifa aliyoitoa kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa madai ya upande wa Marekani kwamba Taleban inakusudia kutotekeleza masharti ya makubaliano ya amani na Marekani, hayana msingi wowote. Ameongeza kuwa Taleban inafungamana na ahadi zake zote. Aidha Shaheen ameendelea kufafanua kuwa, madai ya viongozi wa usalama na intelejensia wa Marekani hayana ukweli wowote na hadi sasa mwenendo wa utekelezaji wa mapatano ya Doha unaendelea vizuri.
Siku mbili zilizopita, yaani tarehe sita Machi, maafisa watatu wa intelejensia na usalama wa Marekani kupitia mahojiano na kanali ya televisheni ya NBC walidai kuwa taarifa walizonazo zinaonyesha kwamba kundi la Taleban halina azma ya kutekeleza makubaliano ya amani yaliyotiwa saini kati ya kundi hilo na Washington. Kwa mujibu wa maafisa hao, baada ya kutia saini makubaliano na Marekani mjini Doha Qatar, wanamgambo wa Taliban wameshadidisha mashambulizi dhidi ya askari wa serikali ya Afghanistan.