Mazungumzo ya kundi la Taliban na wawakilishi wa Marekani na NATO
Mullah Baradar, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya kundi la Taliban ameonana na Zalmay Khalilzad, mwakilishi maalumu wa Marekani na Jenerali Austin Scott Miller, kamanda wa wanajeshi wa Marekani na NATO nchini Afghanistan. Mazungumzo hayo yamefanyika katika mji mkuu wa Qatar, Doha.
Katika mazungumzo hayo ya pande tatu kumezungumziwa mchakato wa kubadilishana wafungwa baina ya kundi la Taliban na serikali ya Afghanistan na vile vile mazungumzo baina ya makundi mbalimbali ya nchi hiyo. Kikao hicho cha pande tatu kimefanyika siku moja baada ya kundi la Taliban kuwaachilia huru wafungwa 38 wa serikali ya Afghanistan.
Kwa mujibu wa makubaliano ya tarehe 29 Februari 2020 baina ya kundi la Taliban na Marekani yaliyofikiwa nchini Qatar, inabidi kabla ya kuanza mazungumzo ya amani baina ya makundi ya Afghanistan, serikali ya Kabul iwaachilie huru wafungwa 5000 wa kundi la Taliban na kundi hilo nalo liwaachilie huru wafungwa elfu moja wa serikali.
Baada ya kukataliwa matakwa ya Taliban ya kuachiliwa kwa mkupuo mmoja wanachama wake elfu tano katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, hivi sasa Taliban inafanya juhudi za kufanikisha matakwa yake hayo kwa kutumia njia ya mazungumzo na mashambulizi ya kijeshi kwa wakati mmoja.
Katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, kundi la Taliban limeongeza mashambulizi yake kwenye maeneo tofauti ya Afghanistan kwa lengo la kuishinikiza serikali ya Kabul kuwaachilia huru wanachama wote wa kundi hilo.
Tab'an kundi la Taliban wakati huo huo linafanya mazungumzo na viongozi wa Marekani ili waishinikize serikali ya Afghanistan iwaachilie huru wafuasi wa kundi hilo.
Katika mazungumzo yake na kundi la Taliban huko Qatar, Marekani iliahidi kuwa, wanachama wote wa kundi hilo wataachiliwa huru hata kabla ya kuanza mazungumzo baina ya makundi ya Afghanistan, hata hivyo serikali ya Kabul imekataa kutekeleza jambo hilo ikisisitiza kwamba, kwanza haikushirikishwa kwenye mazungumzo ya Taliban na Marekani na pia jambo hilo halitokuwa na faida yoyote kwa serikali, bali faida pekee itakuwa ni kwa kundi la Taliban na Marekani.
Kwa kuzingatia kuwa ahadi za Marekani zimechukua muda mrefu kutekelezwa au kwa lugha nyingine, Washington imeshindwa kuikinaisha serikali ya Afghanistan kuwaachilia huru wafuasi wa Taliban, sasa hivi viongozi wa kundi hilo wameingia hofu ya kujirudia mchezo wa kila siku wa Marekani wa kutoa ahadi hewa hasa kwa vile viongozi wa White House ni mabingwa wa kutotekeleza ahadi wanazotoa na kuvunja mikataba ya kimataifa. Wasiwasi wa kutotekeleza Marekani ahadi zake kwa kundi la Taliban unapata nguvu hasa kwa kuzingatia kuwa hivi sasa udhaifu wa serikali ya Washington umezidi kuonekana kutokana na kushindwa kudhibiti ugonjwa wa corona kwa miezi kadhaa sasa. Si hayo tu, lakini pia wimbi la maandamano na machafuko limetandaza kiwingu chake katika miji mbalimbali ya Marekani huku rais wa nchi hiyo Donald Trump akikabiliwa na mtihani mwingine, nao ni uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba 2020. Migogoro hiyo ya ndani ya Marekani imemfanya Trump azingatie zaidi namna ya kujitatua kwanza na migogoro hiyo na kutoyapa kipaumbele masuala mengineyo kama ya amani ya Afghanistan.
Ni kwa kuzingatia hali hiyo ndio maana wachambuzi wa mambo wakasema kuwa, mazungumzo ya mkuu wa ofisi ya kisiasa ya kundi la Taliban nchini Qatar na wawakilishi wa Marekani na NATO huko Afghanistan, ni aina fulani ya onyo ya kundi hilo kwa Marekani na NATO kuhusu madhara ya kucheleweshwa utekelezaji wa ahadi za Marekani au kutotekelezwa kabisa ahadi hizo kulingana na makubaliano ya Doha.
Vile vile inaonekana kwamba, kushiriki makamanda wa kijeshi wa Marekani na NATO katika kikao hicho cha pande tatu huko Doha Qatar, ni ishara kuwa, mazungumzo hayo yamejadili pia suala la kutoka wanajeshi wa kigeni nchini Afghanistan suala ambalo ni miongoni mwa vipengee vya makubaliano ya Doha baina ya Marekani na kundi la Taliban.