China yapinga kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran
Kwa mara nyingine tena China imepinga vikali njama za Marekani za kutaka kurefushwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran. Muda wa vikwazo hivyo unafikia tamati Oktoba mwaka huu wa 2020, kwa mujibu wa Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika ujumbe wa Twitter jana Ijumaa, ubalozi wa China katika Umoja wa Mataifa umeashiria kuhusu barua ya Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ya Asia, Wang Yi aliyomwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo hapo tarehe 7 mwezi huu wa Juni inayosema kwamba: "Baada ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani haina tena haki ya kuwasilisha mashtaka dhidi ya Iran kwa mujibu wa makubaliano hayo."
Katika barua hiyo, Wang Yi ameeleza bayana kuwa, "China inataka kutekelezwa kwa umakinifu vipengee vyote vya Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kikiwemo kipengee kinachohusu marufuku ya silaha."
Waziri wa Mambo ya Nje wa China amekumbusha kuwa, Marekani ilichukua uamuzi wa upande mmoja wa kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa mwaka 2018 sambamba na kurejesha vikwazo vyake haramu dhidi ya Iran, hatua ambazo zinakiuka azimio hilo la Baraza la Usalama.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa China ameitaka Marekani iiondolee Iran vikwazo vyake haramu na ambavyo havina misingi ya sheria za kimataifa, sambamba na kurejea katika njia sahihi ya kuheshimu JCPOA na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inadai kuwa, imeanzisha mkakati huo mpya wa kuhakikisha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran vinaendelea ili kuzuia kile inachodai ni nchi hii kumiliki silaha za nyuklia. Hii ni katika hali ambayo Iran imesisitiza mara nyingi kwamba haijawai kuwa na nia ya kuunda silaha za nyuklia na wala haina mpango wa kumiliki silaha hizo angamizi.