Umoja wa Ulaya: Mgogoro wa Libya hauna utatuzi wa kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61768-umoja_wa_ulaya_mgogoro_wa_libya_hauna_utatuzi_wa_kijeshi
Msemaji wa mkuu wa siasa za nje wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kwamba mgogoro wa Libya hauwezi kutatuliwa kwa njia ya kijeshi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2020 02:37 UTC
  • Umoja wa Ulaya: Mgogoro wa Libya hauna utatuzi wa kijeshi

Msemaji wa mkuu wa siasa za nje wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kwamba mgogoro wa Libya hauwezi kutatuliwa kwa njia ya kijeshi.

Kwa mujibu wa televisheni ya Sky News ya Kiarabu Peter Stano, Msemaji wa Joseph Borell, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya alisema jana Jumatatu kwamba makundi yote yanayopigana nchini Libya yanapasa kusimamisha vita mara moja na kufanya mazungumzo ya kutatua hitilafu zao.

Luigi Di Maio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia na mwenzake wa Ujerumani Heiko Maas, baada ya kufanya mazungumzo huko Rome, mji mkuu wa Italia, walisema kuwa kuna uadharura wa kusitishwa vita mara moja nchini Libya kwa kutilia maanani onyo la hivi karibuni la Misri kuhusiana na nchi hiyo.

Luigi Di Maio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia

Matamshi hayo yametolewa baada ya Rais Abdufattah as-Sisi wa Misri kukitembelea kituo kimoja cha kikosi cha majini cha nchi hiyo kilicho karibu na mpaka wa Libya siku ya Jumamosi na kuonya kuwa nchi hiyo inaweza kuingilia moja kwa moja kijeshi katika mgogoro wa Libya.

Serikali ya Mapatano ya Kitaifa ya Libya GNA siku ya Jumapili ilitangaza kukasirishwa na matamshi hayo ya kichokozi ya rais wa Misri na kusema ni aina fulani ya kutangaza vita dhidi ya Libya.