Indhari ya Imran Khan kuhusu mauaji ya Wakashmiri
https://parstoday.ir/sw/news/world-i62173-indhari_ya_imran_khan_kuhusu_mauaji_ya_wakashmiri
Waziri Mkuu wa Pakistan ametahadharisha kuhusu mauaji ya Wakashmiri yanayofanywa na wanajeshi wa India.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jul 13, 2020 05:45 UTC
  • Indhari ya Imran Khan kuhusu mauaji ya Wakashmiri

Waziri Mkuu wa Pakistan ametahadharisha kuhusu mauaji ya Wakashmiri yanayofanywa na wanajeshi wa India.

Imran Khan ameashiria hali mbaya ya raia wa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India na kueleza kuwa maafa kama kuuliwa kidhulma na Waserbia Waislamu wa Bosnia Herzegovina huko Sebrenica yanawasubiri watu wa Kashmir. 

Waziri Mkuu wa Pakistan ameongeza kuwa wanajeshi wa India wanawauwa kwa umati raia wa Kashmir bila hata ya kuhofia kufuatiliwa kisheria. Imran Khan amebainisha kuwa, raia wa Kashmir zaidi ya milioni 8 wamezingirwa na wanajeshi wa India laki nane; na ni karibu mwaka mmoja sasa raia hao wameshindwa hata kudhaminiwa mahitaji yao ya msingi. 

Mauaji ya umati ya Waislamu wa Sebrenica  

Indhari hii mpya ya Imran Khan kuhusu vitisho vilivyoko dhidi ya Waislamu wa Kashmir eneo linalodhibitiwa na India vinavyotekelezwa na askari usalama wa nchi hiyo ni katika fremu ya mchakato ambao umewekwa katika ajenda yake ya kazi na serikali ya New Delhi tangu msimu wa joto uliopita kwa hatua yake ya kuondoa mamlaka ya kujitawala hususan kwa eneo la Kashmir. 

Chama tawala India cha Baratiya Janata (BJP) ambacho kinaendesha siasa za mielekeo na misimamo ya kitaifa ya uchupaji mipaka katika miongo ya karibuni kimeonesha rekodi hasi sana ya namna inayoamiliana na Waislamu. Tukio chungu na la ukatili la kuharibiwa msikiti wa Baber katika jimbo la Gujerat mwaka 1992 lilifanywa na Wahindu wenye misimamo mikali  wakati wa  utawala wa Waziri Mkuu wa hivi sasa wa India Narendara Modi kulipelekea kuuliwa zaidi ya watu elfu mbili. Mauaji hayo ya kikatili bado hayajafutika katika vinywa vya jamii ya Waislamu wa India.  

Chama cha Narendra Modi cha BJP kimekuwa kikishinda katika chaguzi za bunge za India kuanzia mwaka 2014 na hivyo kuendelea kuongoza nchi. Kuanzia mwaka jana serikali ya nchi hiyo ililifanya suala la kuwawekea Waislamu wa nchi hiyo mashinikizo ya hali ya juu hususan Waislamu wa Kashmir kuwa moja ya ajenda zake kuu. 

Narendara Modi, Waziri Mkuu wa India  

 Hali ya usalama katika eneo la Kashmir imezidi kuwa mbaya baada ya serikali ya India kuliondolea eneo leneo hilo mamlaka ya kujitawala karibu mwaka mmoja sasa;  huku njia za mawasiliano ya simu na Intaneti za wakazi wa eneo hilo zikibanwa kupindukia.  

Serikali ya India aidha imewekea mipaka na vizuizi sherehe na shughuli zote za kidini za Waislamu katika kalibu ya sheria mpya ya uraia ambayo inahesabiwa kuwa ni moja ya vielelezo vya ubaguzi wa kidini huku utoaji wa vibali vya kuishi nchini humo ukiwezekana tu kwa raia wahajiri ambao si Waislamu; hatua ambayo inadhihirisha namna Waislamu wanavyobaguliwa na kunyanyaswa waziwazi huko India. 

Aidha hali ya wasiwasi imeongezeka kufuatia hatua za ukandamizaji na mauaji zinazochukuliwa na polisi wa India dhidi ya Waislamu wa Kashmir kama vifungo vya nyumbani walivyowekewa Waislamu hao. 

Waislamu wa eneo la Kashmir  

Kwa msingi huo Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan ametahadharisha kuhusu mauaji makubwa yanayoweza kufanywa  na askari usalama wa India kwa raia wa Kashmir na kutoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuipa umuhimu kadhia ya Kashmir na hali mbaya sana waliyo nayo raia katika eneo hilo. 

Tunapaswa kuzingatia pia kuwa mashinikizo na vitisho vya kuuliwa Waislamu huko India haviishii tu katika eneo la Kashmir linalohibitiwa na India.  Kuchomwa moto misikiti isiyopungua kumi ni miongoni mwa hatua nyingine zilizo dhidi ya binadamu na za chuki dhidi ya Uislamu zilizochukuliwa na  Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada nchini India. Polisi na askari kulinda usalama wa raia wa nchi hiyo pia nao wamekuwa watazamaji tu mbele ya vitendo hivyo vya kikatili.