Mary Trump: Rais Trump ni mtu hatari, anapaswa kujiuzulu
Mpwa wa Donald Trump amesema rais huyo wa Marekani ni mtu hatari ambaye anapaswa kujiuzulu wadhifa wake wa urais mara moja.
Mary Trump alisema hayo jana Jumatano katika mahojiano na kanali ya televisheni ya ABC News na kuongeza kuwa, "mjomba yangu (Trump) hawezi kabisa kuiongoza nchi na ni jambo la hatari kuruhusu hilo lifanyike."
Mary Trump amesema hayo katika mahojiano yake ya kwanza kabisa baada ya kufanikiwa kuchapisha kitabu kinachoeleza wazi wazi udhaifu na mapungufu ya Trump, licha ya pingamizi kutoka kwa familia ya rais huyo wa Marekani ambayo hapo kabla ilienda mahakamani kusimamisha uzinduzi wa kitabu hicho.
Mpwa huyo wa Trump amesema kiongozi huyo wa Marekani ni mtu asiye na utu wala huruma, na amekuwa akiwatumia watu wakiwemo wanawe na mkewe kama vyombo tu vya kufikia maslahi yake.
Amebainisha kuwa, katu hatanyamaza kimya na kutazama Trump akiivunja na kuisambaratisha Marekani kwa tabia zake zisizoeleweka.
Kitabu cha Mary Trump kimemsawiri Trump kama mtu mwenye hulka zisizo za kawaida, mwenye uchu, tamaa na asiyetosheka; tabia ambazo zinashabihiana na za babake, Fred Trump, aliyefariki dunia mwaka 1999.