CIA yakadhibisha madai ya Trump dhidi ya China kuhusu TikTok
(last modified Mon, 10 Aug 2020 04:24:51 GMT )
Aug 10, 2020 04:24 UTC
  • CIA yakadhibisha madai ya Trump dhidi ya China kuhusu TikTok

Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) limetangaza kuwa halina ushahidi wowote unaothibitisha kwamba serikali ya China inapata taarifa binafsi za raia wa Marekani kupitia mtandao wa kijamii wa TikTok.

Gazeti la New York Times limeripoti kuwa, wachambuzi wa shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, wameandika katika ripoti iliyotumwa White House kwamba "hakuna ushahidi wowote" unaothibitisha kwamba serikali ya China imefanya jitihada za kudukua na kupata taarifa binafsi za watumia wa mtandao wa TikTok. 

Ripoti hiyo ya CIA imetolewa katika kipindi ambacho maafisa wa serikali ya Donald Trump wanapanga kuipiga marufuku aplikesheni maarufu ya video ya TikTok inayomilikiwa na China nchini Marekani.

Maafisa wa usalama wa Marekani wanadai kwamba aplikesheni hiyo ya kampuni ya ByteDance ya China, inatumiwa kukusanya data binafsi za raia wa Marekani.

TikTok imekanusha madai kwamba, inadhibitiwa au inashirikisha data zake na serikali ya China. Jumanne ya wiki hii kampuni hiyo inatarajiwa kuwasilisha mashtaka ya kupinga amri ya Donald Trump.

Aplikesheni hiyo ambayo imepata ushawishi kwa haraka ina watumiaji karibu milioni 80 kila mwezi nchini Marekani na marufuku hiyo itakuwa pigo kubwa kwa kampuni ya ByteDance.

Hivi karibuni, mivutano na mikwaruzano kati ya Marekani na China imeongezeka kutokana na sera za ubinafsi, ubabe na utumiaji mabavu za Washington.