Erdogan: Safari ya Macron nchini Lebanon ilikuwa na malengo ya kikoloni
https://parstoday.ir/sw/news/world-i62809-erdogan_safari_ya_macron_nchini_lebanon_ilikuwa_na_malengo_ya_kikoloni
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ana malengo ya kikoloni nchini Lebanon na kwamba safari yake ya siku chache zilizopita mjini Beirut ilifanyika kwa shabaha ya kutunisha misuli.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Aug 14, 2020 06:32 UTC
  • Recep Tayyip Erdoğan
    Recep Tayyip Erdoğan

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ana malengo ya kikoloni nchini Lebanon na kwamba safari yake ya siku chache zilizopita mjini Beirut ilifanyika kwa shabaha ya kutunisha misuli.

Matamshi hayo ya Erdogan yametolewa huku nchi hizo mbili zikiwa kwenye mvutano na malumbano makali  kuhusu kadhia ya kutafuta gesi katika Bahari ya Mediterrania. 
Erdogan ameuambia mkutano wa viongozi wa Chama cha Uadilifu na Ustawi mjini Ankara kwamba Emmanuel Macron anataka kurejesha ukoloni nchini Lebanon na kwamba kitendo cha kutunisha misuli mbele ya vyombo vya habari hakiishtui Uturuki.
Wiki iliyopita Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitembelea Beirut katika ziara iliyopegiwa debe sana na vyombo vya habari vya Kimagharibi baada ya mlipuko mkubwa uliotokea katika mji huo mkuu wa Lebanon na kuua watu wasiopungua 171. Zaidi ya watu wengine 6,500 walijeruhiwa katika mlipuko huo.
Lebanon ilikoloniwa na Ufaransa tangu mwaka 1920 hadi 1943.
Matamshi ya Rais wa Uturiki dhidi ya Emmanuel Macron yanafuatia mvutano mkubwa uliojitokeza baina ya Ankara na Paris juu ya operesheni inayofanywa na serikli ya Uturuki ya kutafuta gesi katika Bahari ya Mediterania, na kadhia ya Libya. Operesheni ya kutafuta gesi katika eneo hilo imeikasirisha Ugiriki na Umoja wa Ulaya. 

Emmanuel Macron na Erdogan

Paris pia imelaani operesheni hiyo ya Uturuki na imeamua kuimarisha uwepo wa majeshi ya Ufaransa katika eneo la Bahari ya Mediterania kwa kutuma ndege na meli za kivita katika eneo hilo.