Aug 28, 2020 10:12 UTC
  • Msimamo wa kukinzana wa Marekani kuhusu mgogoro wa nyuklia wa Korea

Takriban ni miongo 7 sasa ambapo Marekani ina wanajeshi wake katika Rasi ya Korea. Licha ya kufanyika mazungumzo mara kadhaa baina ya viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini kuhusu kupokonywa silaha za nyuklia Pyongyang lakini mgogoro wa Korea mbili bado uko vile vile. Si hayo tu lakini rais wa Marekani, Donald Trump hivi sasa anataka kupunguzwa idadi ya wanajeshi wa nchi hiyo huko Korea Kusini, suala ambalo limezusha mzozo mpya.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Mark Esper, siku ya Jumatano alisema katika sherehe maalumu huko Hawaii kwamba Marekani itaendelea na msimamo wake wa kufuatilia kupokonywa kikamilifu silaha za nyuklia Korea Kaskazini na wakati huo huo amesema, jeshi la Marekani linapaswa kuwekwa katika hali ya tahadhari ya kukabiliana na Korea Kaskazini. Hapo hapo akasema pia kuwa, njia za kidiplomasia zinaweza kuondoa mkwamo uliopo baina ya Marekani na Korea Kaskazini, matamshi yanayogongana ambayo watu wengi wanawaona viongozi wa Marekani ni wapayukaji na hawajui wanachokisema.

Justin Bronk mtalamu wa masuala ya kijeshi amesema kuwa, Marekani haiwezi kutumia nguvu zozote za kijeshi kukabiliana na Korea Kaskazini bila ya kujikubalisha kwanza kupata hasara kubwa na kujitumbukiza kwenye hatari kubwa.

Sisitizo la Waziri wa Ulinzi wa Marekani kwamba nchi hiyo imeliweka jeshi lake katika hali ya tahadhari kwa ajili ya kupambana na Korea Kaskazini kwa madai ya eti kulinda usalama wa waitifaki wa Marekani, linakinzana na madai yake kuwa Marekani inapenda kutumia njia za kidiplomasia kutatua mgogoro wake na Korea Kaskazini. Mgongano zaidi unajitokeza pale tunapozingatia kuwa sera za Marekani ni kupunguza idadi ya wanajeshi wake katika Rasi ya Korea lakini wakati huo huo Washington inadai kuwa inajiimarisha kijeshi kukabiliana na Korea Kaskazini. 

Mazungumzo ya kimaonesho baina ya Marekani na Korea Kaskazini

 

Ukweli ni kuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani yuko chini ya mashinikizo ya rais wa nchi hiyo, Donald Trump ya kuondoa wanajeshi wa Marekani nchini Korea Kusini. Sisitizo hili  la Trump nalo linakinzana na madai yake kwamba yuko tayari kulinda usalama wa waitifaki wake katika eneo la Asia Mashariki.

Kuendelea mzozo baina ya afisa huyo wa ngazi za juu zaidi wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani na Donald Trump huenda kukaishia kwenye yaliyomfika James Mattis, waziri wa kwanza wa ulinzi katika serikali ya Trump ambaye alitimuliwa kwenye cheo hicho baada ya kutofautiana na Trump kuhusu kutoka wanajeshi wa Marekani nchini Syria.

Mwaka 2019, serikali ya Trump iliishinikiza Korea Kusini kwamba iongeze kwa kiwango kikubwa malipo yake ya kugharamia kuweko makumi ya maelfu ya wanajeshi wa Marekani nchini humo na ilitishia kuwa kama Seoul itakataa kuongeza kiwango hicho basi Marekani itaondoa wanajeshi wake nchini humo. 

Msimamo wa Trump ni kwamba waitifaki wa Washington huko Asia Mashariki ikiwemo Korea Kusini ni sawa na kasha la fedha ambalo linatumika kununua silaha za Marekani na kuweka mikataba ya kila namna ya kiuchumi na nchi hiyo sambamba na kugharamia uwepo wa wanajeshi wa Marekani katika nchi hizo. Trump anatamka wazi kuwa kasha hilo la fedha (yaani nchi vibaraka wa Marekani Asia Mashariki) lazima litumike kadiri inavyowekezana kwa manufaa ya kifedha na kiuchumi ya Marekani.

Mark Esper, Waziri wa Ulinzi wa Marekani

 

Hata hivyo Korea Kusini inaamini kuwa, fedha ambazo inalipa kugharamia kuweko wanajeshi wa Marekani nchini humo kiwango chake ni kikubwa sana. Ni zaidi ya mara kadhaa ya kiwango kinacholipwa na nchi za Ulaya kugharamia kuweko wanajeshi wa Marekani barani humo.

Hivi sasa kuna wanajeshi 28 elfu na 500 wa Marekani huko Korea Kusini. Trump anataka Korea Kusini ilipe dola bilioni 5 kila mwaka kugharamia kuweko wanajeshi hao nchini humo. Hicho ni kiwango wa fedha cha mwaka 2018 ambacho kilionesha ongezeko la mara tano zaidi ikilinganishwa na kiwango cha kabla yake.

Korea Kusini imependekeza kuongeza asilimia 13 ya fedha inazogharamia uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini humo lakini Washington inasema fedha hizo hazitoshi msimamo ambao umezitumbukiza kwenye mkwamo nchi hizo ambazo kidhahiri zinaonekana ni marafiki. 

Tags