Trump afunguliwa mashitaka kwa kuiwekea vikwazo mahakama ya ICC
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63775-trump_afunguliwa_mashitaka_kwa_kuiwekea_vikwazo_mahakama_ya_icc
Mawakili mashuhuri wa kutetea haki za binadamu wameufungulia mashitaka utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kwa hatua yake ya hivi karibuni ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 02, 2020 08:04 UTC
  • Trump afunguliwa mashitaka kwa kuiwekea vikwazo mahakama ya ICC

Mawakili mashuhuri wa kutetea haki za binadamu wameufungulia mashitaka utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kwa hatua yake ya hivi karibuni ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Mawakili hao wamesema hatua hiyo ya mwezi Juni mwaka huu ya utawala wa Washington ya kutangaza vikwazo dhidi ya Mkuu wa Mashtaka wa korti hiyo, Fatou Bensouda na afisa mwingine wa ngazi ya juu Phakiso Mochochoko imesitisha kazi zao za kushughulikia kesi za jinai.

Mmoja wa mawakili hao, Diane Marie Amann, Profesa wa Sheria ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Georgia amesema, "dikrii hiyo ya Trump ni ya kipumbavu na isiyozingatia utawala wa sheria. Nafanya kazi kwa niaba ya watoto walioathiriwa na migogoro ya kivita, waliouawa, waliokabiliwa na mateso, waliobakwa, waliolazimishwa kuwa wanajeshi licha ya umri wao mdogo na waliouzwa kama bidhaa, lakini hivi sasa siwezi tena!"

Shirika la kutetea haki za binadamu la Open Society Justice limesema uamuzi huo wa Trump wa kuwawekea vikwazo maafisa wa ngazi za juu wa ICC si tu umekiuka katiba ya Marekani, lakini pia umesaliti 'uungaji mkono wa muda mrefu wa Washington' kwa mfumo wa sheria ya kimataifa.

Fatou Bensouda na Phakiso Mochochoko

Mahakama hiyo ya kimataifa yenye makao yake The Hague, Uholanzi imebainisha kuwa, vikwazo hivyo vilivyotangazwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo dhidi ya Fatou Bensouda na Phakiso Mochochoko ni "hujuma nzito" dhidi ya utawala wa sheria.

ICC imesema kitendo hicho cha Washington ni jaribio jengine la kuingilia uhuru wa mahakama hiyo wa kuchunguza na kuendesha kesi, lakini imesisitiza kuwa itaendelea na uchunguzi wake kuhusiana na jinai zilizofanywa na Marekani na waitifaki wake nchini Afghanistan.