Oct 09, 2020 10:35 UTC
  • Ahadi mpya za Trump za kuondoa wanajeshi Afghanistan; ahadi chapwa za kiuchaguzi

Uchaguzi wa Rais nchini Marekani unazidi kukaribia huku hali ya kisiasa ya rais wa nchi hiyo, Donald Trump si nzuri mbele ya mpinzani wake Joe Biden. Ikulu ya White House na hasa Trump mwenyewe wanazidi kufanya lolote liwezekanalo, hata kutoa ahadi za maneno tena zenye migongano, ili kuvutia wapiga kura.

Ahadi za karibuni kabisa ni hizi zilizotolewa na Trump za kuhakikisha wanajeshi wote wa Marekani wameondoka nchini Afghanistan ifikapo mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu. Siku ya Alkhamisi, Trump aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba wanajeshi wote wa Marekani waliobakia huko Afghanistan watarejea nyumbani wakati wa X-Mass mwaka huu. Hata hivyo uzandiki wa Trump na viongozi wa Marekani umeonekana wazi katika maneno hayo kwani usiku wa kuamkia hiyo hiyo Alkhamisi, Robert O'Brien, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Trump alisema kuwa, wanajeshi wa Marekani hawataondoka Afghanistan kiasi kwamba ifikapo mwanzoni mwa mwaka 2021, wanajeshi 2,500 wa nchi hiyo watabakia nchini humo.

Cha kushangaza ni kwamba hata kundi la Taliban la Afghanistan limeelezea kufuruhishwa na ahadi hizo za Trump na kudai kuwa hiyo ni hatua nzuri ya utekelezaji wa makubaliano ya Doha. Itakumbukwa kuwa, mwezi Februari 2020 serikali ya Trump ilifikia makubaliano na kundi la Taliban mjini Doha Qatar na pande mbili zilikubaliana kwamba hadi kufikia mwezi Mei 2021, wanajeshi wote wa kigeni watakuwa wameshaondoka nchini Afghanistan. Kwa upande wake, Taliban iliahidi kusimamisha vita na kufanya mazungumzo na serikali ya Afghanistan kuhusu kugawana madaraka. 

Wanajeshi wa Marekani katika mashamba ya madawa ya kulevya nchini Afghanistan

 

Kabla ya hapo, Trump alikuwa amedai kwamba ifikapo mwezi Novemba 2020 wanajeshi wa Marekani watapunguzwa na kufikia elfu nne hadi elfu tano huko Afghanistan. Kuwarejesha nyumba wanajeshi wa Marekani walioko nchini Afghanistan ilikuwa ni ahadi kuu ya Trump wakati wa uchaguzi uliopita. Katika matamshi yake ya Jumatano usiku, O'Brien, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Ikulu ya Marekani, White House alidai kuwa, wakati Trump alipoingia madarakani, wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan walikuwa ni zaidi ya elfu kumi, lakini sasa hivi wamebakia chini ya elfu tano na ifikapo mwanzoni mwa mwaka ujao, watabakia 2,500. Tunapoyaangalia matamshi haya ya O'Brien tutaona yanapingana wazi na madai ya Trump aliyesema kuwa, wanajeshi wote wa Marekani watakuwa wameondoka Afghanistan ifikapo tarehe 25 Disemba mwaka huu wa 2020. Cha kushangaza zaidi ni kuwa, Trump na mshauri wake wa usalama wa taifa wanakuwa na vikao vya mara kwa mara vya kiusalama, lakini pamoja na hayo wanashindwa hata kupangilia vizuri maneno yao ili yasigongane. Ni kwa sababu pia hii ndio maana wachambuzi wa mambo wakasema, lengo pekee la matamshi ya viongozi hao wa Marekani ni kudanganya walimwengu na kuvutia kura za Wamarekani tu. 

Kwa kweli matamshi mapya ya Trump ya kwamba wanajeshi wote wa Marekani wataondoka nchini Afghanistan tena hata kabla ya kufika muda waliokubaliana na kundi la Taliban, ni ahadi chapwa za kujaribu kumwokoa Trump katika hali mbaya ya kisiasa na kiuchaguzi aliyo sasa hivi huko Marekani. Zamir Kabulov, mwakilishi wa Russia katika kadhia ya Afghanista amejibu madai hayo mapya ya Trump kwa kusema: Matamshi hayo y Trump yanawalenga zaidi wapiga kura ndani ya Marekani hayana kitu chochote cha maana.

Maelfu ya wanajeshi wa Marekani wameshauawa na kujeruhiwa nchini Afghanistan

 

Suala jingine muhimu ni kwamba, kwa kuzingatia kuwa umebakia chini ya mwezi mmoja hadi kufikia wakati wa uchaguzi wa rais huko Marekani, haijulikani kwamba Trump atashinda au atashindwa. Hivyo hakuna dhamana yoyote ya kutekelezwa ahadi alizotoa siku ya Alkhamisi hasa iwapo atakayeingia madarakani baada ya uchaguzi huo atakuwa mtu mwingine.

Aidha ni vyema kusema kuwa, tangu Marekani ilipoivamia Afghanistan ambapo siku ya Jumatano uvamizi huo wa Afghanistan ulitimia miaka 19, hakuna matunda yoyote ya maana yaliyopatikana. Hadi sasa karibu wanajeshi 2,400 wa Marekani wameshauawa nchini humo na maelfu ya wengine wameshajeruhiwa. Baya zaidi ni kwamba kuweko wanajeshi wa Marekani na NATO huko Afghanistan hakujazaa matunda mengine isipokuwa kuuliwa bila sababu wananchi wa nchi hiyo, kuongezeka machafuko na ukosefu wa usalama pamoja na ongezeko kubwa kupindukia la uzalishaji wa madawa ya kulevya.

Tags