Majanga ya kimaumbile yaongezeka maradufu duniani kote
Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imebaini kuwa majanga ya kimaumbile yameongezeka maradufu katika kipindi cha miaka 20 iliyopita huku mabadiliko ya tabianchi yakitajwa kuwa sababu kuu ya hali hiyo.
Ripoti hiyo iliyotolewa mjini Geneva Uswisi na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza madhara ya majanga, UNDRR imesema kati ya mwaka 2000 na 2019 kulikuwepo matukio 7348 ya majanga yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 1.2 huku watu wengine bilioni 4.2 wakiathiriwa kimaisha na majanga hayo.
Gharama za majanga hayo ni dola trilioni 2.9 ambapo ofisi hiyo imesema kiwango hicho cha hasara na vifo ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na matukio ya miaka 20 iliyopita ambapo kulikuwepo matukio 4,212.
Tofauti hiyo kubwa imetajwa kusababishwa na ongezeko la majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mfano matukio ya mafuriko kati ya mwaka 1980 na 1999 yalikuwa 1389 ikilinganishwa na 3254 kati ya mwaka 2000 na 2019. Ripoti hiyo imemulika pia ukame, mioto ya nyika na viwango vya juu zaidi vya joto. Matetemeko ya ardhi na tsunami nayo pia yametajwa kusababisha vifo vya binadamu kuliko majanga mengine ya asili.
Wakati huo huo, ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kupunguza hatari ya majanga, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametahadharisha kuwa janga la COVID-19 limeleta umakini mpya kuhusu umuhimu wa kuimarisha upunguzaji wa hatari za majanga kwani hali inazidi kuwa mbaya pindi panapokosekana udhibiti mzuri wa hatari za majanga.