Maandamano yaendelea Paris Ufaransa, kupinga ukandamizaji dhidi ya Waislamu
(last modified Mon, 15 Feb 2021 07:52:19 GMT )
Feb 15, 2021 07:52 UTC
  • Maandamano yaendelea Paris Ufaransa, kupinga ukandamizaji dhidi ya Waislamu

Maandamano ya wananchi wa Ufaransa ya kupinga sheria kali za kuwakandamiza Waislamu nchini humo yanaendelea hasa dhidi ya mpango mpya wa nchi hiyo ya kuwabana zaidi ya Waislamu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, mji mkuu wa Ufaransa, Paris jana ulishuhudia maandamano ya kupinga mpango wa serikali ya nchi hiyo wa kutaka kuweka sheria za kuwabana zaidi Waislamu.

Jumanne iliyopita wabunge ya Ufaransa walipasisha muswada wa sheria hiyo na kuna uwezekano mkubwa mabunge yote mawili ya nchi hiyo nayo yataupasisha.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amedai kuwa, ni jambo la dharura kupasishwa sheria hiyo kwani inalinda thamani za nchi hiyo kama vile usawa wa kijinsia na mfumo wa kisekula unaopinga dini kuwa na nafasi katika maisha ya mwanadamu. Amedai pia kuwa sheria hiyo itang'oa fikra za kuchupa mipaka.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron

 

Hata hivyo waandamanaji nchini Ufaransa wanasema kuwa serikali ya Paris inatumia sheria hiyo kwa ajili ya kuwanyanyasa na kuwakandamiza zaidi Waislamu ambao idadi yao ni ya pili kwa ukubwa katika nchi hiyo ya Ulaya.

Katika miezi ya hivi karibuni, serikali Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa imechukua hatua nyingi za kuwakandamiza na kuwanyanyasa Waislamu.